BIASHARA MASHINANI: Aliona rafikiye akisaka viazisukari dukani, akapata wazo la kuvikuza
Na PETER CHANGTOEK
ALILELEWA na wazazi waliokuwa na ujuzi kuhusu masuala ya kilimo.
Mamake alikuwa afisa wa kilimo wa nyanjani, ilhali babake alikuwa ameenda nchini Uingereza kusomea masuala ya usimamizi wa mifugo, na hivyo basi kuwa na ujuzi katika uga wa zaraa.
Japo Robert Muturi alisomea shahada ya elimu (Uchumi na Biashara), ameamua kuzifuata nyayo za wavyele wake, kwa kushughulika na kilimo. Ama kwa kweli mwana hutazama kisogo cha nina anapobebwa mgongoni!
Yeye hujishughulisha na shughuli ya ukuzaji wa mimea ya viazisukari (beetroots) katika Kaunti Ndogo ya Kieni Magharibi, Kaunti ya Nyeri.
Anasema kuwa hapo awali, alikuwa akijihusisha na kilimo cha mboga na matunda, lakini baadaye akabadilisha mawazo yake, baada ya kugundua kuwa viazisukari ni mmea wenye manufaa mengi.
Lakini ni nini kilichomsukuma mkulima huyo hadi akajitosa katika zaraa hino?
Anaeleza kuwa wakati mmoja, alipokuwa ziarani na rafikiye mmoja, alipata fursa ya kuandamana naye katika supamaketi moja, ambapo mwenzake alinunua viazisukari.
“Hapo ndipo nilipotaka kujua zaidi kuhusu jina beetroot. Aliniambia kuwa hutulizwa nazo baada ya uchovu wa siku,” asema, akiongeza kuwa punde si punde, yeye akaingia katika mtandao wa Google na kusoma kuhusu manufaa ya beetroots.
Alipata motisha na kutamani kuanzisha kilimo cha viazisukari. Licha ya kupata habari hizo kutoka mtandaoni, hakujua aanzie wapi amalizie wapi!
“Nilianza kutembelea maonyesho ya kilimo, lakini sikupata jawabu hadi wakati ambapo nilitembelea Wambugu Farm, Nyeri. Walikuwapo wahudumu wa kampuni za mbegu walionipa habari nilizotaka kuzijua kutoka kwao. Hatimaye, nikaanza kwa kulitumia shambo dogo ambapo mimea hiyo ilizalisha mazao tani moja na nusu,’’ afichua mkulima huyo, akiongeza kuwa, aliyauza mazao hayo kwa madalali walionunua kwa Sh40 kwa kilo moja.
Mkulima huyo, kwa wakati huu, ana mimea ya viazisukari katika shamba la ekari thumuni moja (1/8), mimea ambayo imekomaa na kuwa tayari kung’olewa kwa ajili ya kuuzwa.
“Natarajia tani tatu,” asema.
Fauka ya hayo, mkulima huyo ana mimea ya viazisukari katika shamba jingine ambalo ni ekari moja. “Lakini nina uhakika kuwa hivi karibuni wakulima wengi watajitosa katika ukuzaji wa beetroots kwa sababu ni rahisi kukuza na faida ni kubwa,” aongeza.
Anaeleza kuwa ni muhimu kuliandaa shamba vyema, kwa kulilima hadi mchanga uwe mwororo.
“Tengeneza mistari kwa umbali wa sentimita 20 kutoka kwa mstari mmoja hadi mwingine, na upande moja kwa moja shambani. Unatakiwa kuzifunika mbegu kwa mchanga kidogo,” aeleza, akisisitiza kwamba ni muhimu kuzipanda mbegu mwanzoni mwa msimu wa mvua.
“Huchukua muda wa siku kumi kuota, na kutoka hapo unatakiwa kuitunza mimea dhidi ya magugu. Itakapokuwa na kimo cha sentimita 20, unatakiwa kuing’oa baadhi ya mimea hiyo, ili uiachie nafasi ya inchi 6 kutoka kwa mmea mmoja hadi kwa mwingine,’’ aeleza mkulima huyo, akitilia mkazo kuwa mimea yote iliyong’olewa yaweza kutumiwa kuwa mboga, na hivyo basi hakuna hasara.
Muturi, ambaye ni mzawa wa tatu katika familia ya watoto wanne, anafichua kuwa mbegu za viazisukari hupatikana katika maduka mbalimbali ya kuuza mbegu na shamba ekari moja huzihitaji kilo mbili za mbegu. Anaongeza kuwa mja anatakiwa kuzinunua mbegu zenye uwezo wa kustahimili magonjwa.
Japo mkulima huyo anasema kuwa ni muhali mno kwa mimea ya viazisukari kuathiriwa na magonjwa, maradhi hutokea kwa wakati fulani. Hata hivyo, anasema kuwa yeye hajawahi kushuhudia kutokea kwa magonjwa wala wadudu waharibifu na kuidhuru mimea yake shambani.
Kwa mujibu wa mkulima huyo ambaye hukuza viazisukari aina ya Detroit dark-red, mimea hiyo huchukua muda mfupi kukomaa na kuvunwa, na hivyo ni mmea mzuri kukuzwa hata kwenye maeneo yenye mvua kidogo kwa sababu huchukua miezi miwili tu kutoka wakati wa kupandwa.
Kwa mujibu wa mkulima huyo mwenye umri wa miaka 36, kupasuka kwa mchanga unaouzunguka mmea ni ishara inayoashiria dhahiri shahiri kuwa mmea huo uko tayari kuvunwa.
Soko
Mkulima huyo anafichua kwamba lipo soko la viazisukari, maadamu waja wengi wanaendelea kujua kuhusu manufaa ya mmea huo kwa afya ya binadamu. Anaongeza kuwa wauzaji wa sharubati au juisi ndio huinua ununuaji wa viazisukari. Pia, hutumiwa kama saladi.
Muturi anasema kuwa kilo moja ya viazisukari huuzwa kwa kati ya Sh40 na Sh60. Anaamini kuwa shamba ekari moja lafaa kuzalisha tani 50 za viazisukari, endapo kanuni zote za ukulima zitazingatiwa.
Changamoto
Mojawapo ya changamoto ambazo mkulima huyo amezipitia ni kuwa, masoko mengi huhitaji mtu ambaye ana uwezo wa kuzalisha mazao hayo mfululizo, na hivyo kumshurutisha kuwategemea wanunuzi wadogowadogo.
Hata hivyo, anapania kuitumia mikakati kabambe kuhakikisha kuwa kuna uzalishaji wa mwezi baada ya mwezi.
“Ninaweka mipango katika shamba langu ili kuhakikisha kuwa ninazalisha tani kumi kila mwezi,’’ asema Muturi, ambaye mbali na kuikuza mimea ya viazisukari, pia hukuza viazi vya kawaida na mihindi.
Anawasihi wenye nia ya kujitosa na kujibwaga katika kilimo cha viazisukari kufanya hivyo maadamu ni “rahisi, si ghali na huchukua muda mfupi kukuza viazisukari na kuna soko.’’
Manufaa
Kuna manufaa kadha wa kadha ya bitiruti, mathalan kushusha shinikizo la damu mwilini. Hali kadhalika, huweza kuzuia kutokea kwa aina fulani za kansa kwa binadamu.