Habari

Sonko alemaza jiji kwa kufuta kazi maafisa 16

September 26th, 2019 1 min read

Na LEONARD ONYANGO

HUDUMA jijini Nairobi huenda zikatatizika baada ya Gavana Mike Sonko kusimamisha kazi maafisa 16, wakiwemo mawaziri.

Wizara iliyoathiriwa zaidi ni ile ya ujenzi ambapo Sonko amesimamisha maafisa 12.

Gavana Sonko aliwasimamisha kazi maafisa hao baada ya mkasa ambapo jengo la darasa la shule ya Precious Talent mtaani Dagoretti liliporomoka na kusababisha maafa ya wanafunzi saba huku wengine wengi wakijeruhiwa.

Sonko alisimamisha kazi maafisa hao kupisha uchunguzi, kulingana na taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari.

Mawaziri waliosimamishwa kazi ni Bw Charles Kerich aliyekuwa Waziri wa Ardhi na Mipangilio ya Ujenzi kabla ya kuhamishiwa katika Wizara ya Fedha na Bw Mohammed Dagane (Afya na Usalama wa Umma).

Bw Kerich, mhariri mkuu wa zamani wa gazeti la ‘The Star’, amewahi kuhudumu katika wizara nne –Mawasiliano, Ardhi, Afya na Fedha- na aliteuliwa na Bw Sonko kuwa ‘waziri mkuu’ mnamo Julai 2019.

Kerich amekuwa akisimamia wizara zote 10 za serikali ya kaunti na kusimamishwa kwake kutasababisha kuzorota kwa huduma jijini.

Wengine waliosimamishwa kazi ni Katibu wa Wizara ya Mipangilio ya Ujenzi jijini Justus Kathenge ambaye hajakuwa afisini tangu Agosti, mwaka huu.

Bw Kathenge alisimamishwa kazi Agosti kutokana na madai ya kuruhusu ujenzi wa majumba kiholela katika mitaa ya Karen, Kileleshwa na Lavington.

Wengine walioathiriwa ni Jusper Ndeke (Mkurugenzi wa Uhakiki Majengo), Dominic Mutegi (Mkurugenzi wa Maendeleo), Ochanda Ondari Fredrick (naibu Mkurugenzi wa Uhakiki wa Majengo), Ruth Waruguru (mkurugenzi wa Mipangilio ya Ujenzi) na Thomas Dudi (Naibu Mkurugenzi wa Mipangilio ya Ujenzi).