Habari

Matiang'i ahamisha polisi wote wakuu kaunti

September 27th, 2019 1 min read

Na VALENTINE OBARA na LEONARD ONYANGO

WAZIRI wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i amefanya mabadiliko makubwa ya usimamizi wa usalama katika Kaunti ya Kiambu.

Ameahidi kufuata nyayo za aliyekuwa waziri, marehemu John Michuki kupambana na wahalifu wanaohangaisha umma katika eneo hilo.

Alisema hayo jana baada ya mkutano wa wakuu wa usalama wa taifa na kaunti baada ya malalamishi ya viongozi na wakazi kwamba uhalifu umekithiri mno.

Akihutubia wanahabari baada ya mkutano wao uliofanywa faraghani, waziri aliagiza mabadiliko katika usimamizi wa polisi na maafisa wa utawala wa serikali kama vile machifu na manaibu wao.

Vilevile, aliagiza shughuli zianzishwe mara moja kujaza nafasi za machifu na manaibu wao ambazo zimekuwa wazi kwa muda mrefu katika sehemu mbalimbali za Kiambu.

“Nawahakikishia hamtashuhudia visa hivi vya uhalifu tena. Kama yeyote kati yenu anawafahamu wahalifu eneo hili, wajulishe hatutawahurumia kwa sababu wananchi wana haki ya kuendeleza shughuli zao bila kuhangaishwa,” akasema.

Kulingana na Dkt Matiang’i, inashukiwa kuna wanasiasa wanaotumia magenge ya wahalifu kutatiza amani kwa malengo yao.

“Sheria haibagui kwa msingi wa cheo cha mtu. Tutatekeleza sheria kikamilifu,” akasema na kuonya kwamba, atafuata nyayo za Michuki kudumisha usalama.

Bila huruma

Marehemu Michuki anafahamika kwa jinsi alivyokuwa akipambana na wahalifu bila huruma.

Dkt Matiang’i alikuwa ameandamana na waziri wa Maji Simon Chelugui, Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Nzioki Mutyambai, Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Edward Mbugua pamoja na wakuu wa usalama wa Kaunti ya Kiambu.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Naibu Gavana wa Kiambu James Nyoro na Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria.

Mahakama ilimwagiza Bw Waititu kutofika afisini ili uchunguzi kuhusiana na madai ya ufisadi yanayomkabili ufanywe.