Habari

Joho asema amefuta wafanyakazi kwa sababu ya SGR

September 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SIAGO CECE

GAVANA wa Mombasa Hassan Joho kwa mara ya kwanza amesema ameathririka pakubwa na uamuzi wa serikali kusafirisha mizigo kupitia kwa reli ya kisasa (SGR).

Bw Joho alisema kuwa amelazimika kufuta kazi asilimia 90 ya wafanyakazi wake aliowaajiri katika kampuni zake mbili katika sehemu za kuhifadhi shehena (CFS) .

Gavana huyo pia alitofautiana na wanaomkashifu akisema ni yeye aliyepasua mbarika kuhusu madhara ya SGR wakati wa kampeni za 2016.

“Mwaka wa 2016, nilisema kuwa SGR itakuwa na athari kubwa sana kwetu na nilieleza kwa nini. Wakati huo watu walinikejeli na kuniona mjinga. Sasa wao ndio wanapinga SGR baada ya madhara kuonekana,” Bw Joho alisema.

Aliongezea kuwa wapinzani wake wamekuwa wakimlaumu kwa kutozungumzia suala hili kwa muda mrefu.

Hata hivyo, Bw Joho aliwahimiza watu wasiwe na wasiwasi kwani tayari amefanya mazungumzo na Rais Uhuru Kenyatta kuhusu suala hili.

“Nasikitika kuona watu wakihama katika makazi yao wakielekea maeneo mengine kutafuta kazi,” alieleza.

Akiongea katika Chuo cha Kenya Coast National Polytechnic (KCNP), Bw Joho alisema biashara za kibinafsi zinafaa ziachwe zifanye kazi kama zile za umma.

Aidha, Gavana huyo alisema yeye ndiye aliyesaidia eneo la pwani kupata mradi wa Sh40 bilioni wa Dongo Kundu.

“Kwa sasa hakuna vile tutasema kuwa serikali ifunge SGR ambayo ilitumia Sh400 bilioni. Wakati huu tunatafuta mbinu za kuimarisha uchumi wa Mombasa na Pwani,” alieleza.

Awahimiza wakazi wawe watulivu

Aliwahimiza wakazi kuwa watulivu kwa kutafuta njia mbadala za kufanya biashara wakingoja mradi huo umalizike.

Hata hivyo, Bw Joho alisema kuwa mpango wake na mazungumzo kati yake na Rais Kenyatta umesaidia eneo la Pwani kuwa na maendeleo zaidi ikiwemo daraja linalotarajiwa kujengwa eneo la Likoni.

” Nilimueleza Rais kuwa mradi wa Dongo Kundu hautamalizika bila kujenga daraja eneo la Likoni. Huu ni mpango wangu kama kiongozi,” Bw Joho alisema.

Wafanyibiashara ambao wamekuwa wakitumia magari kusafirisha mizigo yao wamekuwa wakilalamika kuwa SGR imekuwa ikiwanyima biashara.

Kutokana na ukosefu wa biashara, wafanyibiashara hao walifanya mandamano huku wakishinikiza Kaunti na Serikali kuu kutafuta njia mwafaka ya kusulushisha swala hili.

Tangu kuanzishwa kwa usafirishaji wa makasha kwa kutumia SGR, wafanyibiashara wamelalamikia mapato duni.