Makala

KINA CHA FIKIRA: Tafsiri za kizuzu adui mkubwa wa lugha ya Kiswahili

October 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na KEN WALIBORA

WAKENYA ni wabunifu sana. Hunishangaza kwa ubunifu wao uliopitiliza.

Hivi punde tu nimemsikia mama mmoja akiniambia, *‘imegwama.’ Je, neno hili *‘gwama’ nalo limetoka wapi? Yaani neno ‘kwama’ lilibadilikaje likawa *‘gwama?’ Kwa kweli hili neno ni ithibati ya ubunifu wa Wakenya; weledi wa kuvumbua kisichowahi kuwapo.

Je, Wakenya hawakubuni ‘M-Pesa’ ambayo kwa kweli tahajia zake zinapaswa kuwa E-M-P-E-S-A? Kosa lao ni kukosa kuliswahilisha barabara na kulitamka “Mpesa” yaani mti unaoota matunda yaitwayo pesa.

Wametuundia mfumo wa uhawilishaji pesa wa M-Pesa na neno EMPESA ambalo sasa limeingia katika kanzi ya maneno ya Kiswahili. Au bado halijaingia?

Isitoshe, Wakenya wamehawilisha maana ya neno ‘mteja,’ neno nililolitumia nilipotafsiri Kiingereza cha ujumbe wa kampuni ya Safaricom, ili kuwa “Mteja wa nambari uliyopiga hapatikani kwa sasa.” Neno ‘mteja’ kwa maana ya mnunuzi wa huduma au bidhaa yoyote popote lilipoteza maana kwa Wakenya wengi likawa linamaanisha mtu asiyepatikana kwa simu.

“Nimekupigia simu, nawe ulikuwa mteja,” utawasikia wakisema. Kwa kweli wanaweza hata wakamgombeza ‘mteja’ kwa kutopatikana au kutopokea simu.

Mara nyingine mimi hujiuliza iwapo nikipigiwa simu nikipokea au nisipoipokea inasalia kuwa simu yangu. Mbona nilaumiwe kwa changu? Ubunifu wa Mkenya ndio unaomsukuma kulihusisha neno mteja na kutokuwapo au kutopokea simu. Ni ubunifu wa ajabu huu, au sio?

Hawa waliotuundia neno *‘gwama’ ndio waliotuundia *‘gwaheri.’ Hawataki kusema ‘kwaheri’ kwa nini? Au ndimi zao nzito, haziwezi kuhimili wepesi wa herufi ‘K.’

Changamoto ya lugha ni kwamba mtu anapokosea huwa aghalabu hana habari kwamba anakosea. Ukimkosoa umekosea wee! Unakiona kilichomfanya sangara kuchomwa moto.

Ukimkosoa anashangaa ghaya ya kushangaa: unamkosoaje kwa jambo ambalo amekuwa analisema kwa miaka na mikaka mpaka akalihalalisha?

“Mazoea yana taabu” walisema waliosema. Wakaongeza kuwa “tabia ni ngozi.” Na kwa ndugu zetu Watanzania, walichozoea sasa ni “mwisho wa siku.”

Utawasikia wakisema, “Anazungukazunguka mume wangu lakini mwisho wa siku atarudi hapa kwangu.” Hii ‘mwisho wa siku’ nayo imetoka wapi? Je, ni tafsiri ya kizuzu ya kauli ya Kiingereza, “at the end of the day?” Kama ndivyo, basi ni balaa bin beluwa.

Nilipokuwa katika hafla ya Kiswahili jijini Arusha mwezi uliopita, gwiji wa tafsiri Prof Hermas Mwansoko alilizungumzia hili akawavunja watu mbavu. Wamezoea kusema ovyoovyo, “mwisho wa siku, mwisho wa siku.” Kwa hiyo mwisho wa siku ni saa ngapi? Je, saa kumi na mbili jioni, saa tatu usiku au saa sita usiku?

Jamani acheni kutusongolea Kiswahili kwa tafsiri za kizuzu. Zamani nikiziita tafsiri sisisi. Lakini kuziita tafsiri sisisi ni kuwapa heshima mno wasemaji wa aina hii ya Kiswahili kombo. Tafsiri sisisi ina utaalamu wake, ila tafsiri ya kizuzu, iwe sisisi au la, inaashiria kiama cha Kiswahili.

Wanaosema *‘mwisho wa siku’ Tanzania na *‘gwama’ Kenya, hatimaye wanakikwamisha Kiswahili.