Michezo

Macho ya Kenya Doha kwa Obiri na Chepng'etich

October 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

NYOTA Hellen Obiri, Lilian Kasait na Margaret Chelimo watakabiliwa na mtihani mkali katika kampeni zao za kufuzu kwa fainali za mbio za mita 5,000 kwa upande wa wanawake.

Obiri ambaye ni malkia wa Afrika, Jumuiya ya Madola na Dunia katika mbio hizo ni mmoja wa watimkaji ambao walitegemewa sana kuzolea Kenya nishani ya dhahabu katika mbio za mita 10,000 mwishoni mwa wiki jana.

Hata hivyo, maazimio hayo yalizimwa na Sifan Hassan wa Uholanzi na Letesenbet Gidey wa Ethiopia. Kenya ililazimika kuridhika na medali ya shaba iliyotwaliwa na Agnes Tirop.

Leo Jumatano, Obiri atakuwa na fursa ya kurejesha matumaini ya Kenya hasa ikizingatiwa ubora wa rekodi ambayo amekuwa akijivunia msimu huu. Zaidi ya kushinda kivumbi cha kilomita 10 kwenye Mbio za Nyika za Dunia nchini Denmark mapema mwaka huu, Obiri pia alimaliza wa pili nyuma ya Tirop katika mbio za kitaifa za mita 10,000 jijini Nairobi mnamo Agosti.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Obiri, 29, kushiriki mbio za mita 10,000 katika ulingo wa kimataifa. Licha kueleza ukubwa wa kiwango cha kufadhaika kwake mwishoni mwa mbio hizo, anapigiwa upatu wa kutinga fainali za mbio za leo Jumatano kwa wepesi na kushindia Kenya medali katika fainali za Oktoba 5.

Kasait atajibwaga ulingoni akijivunia hamasa tele baada ya kutawala mbio za mita 5,000 katika Michezo ya bara la Afrika (AAG) iliyoandaliwa jijini Rabat, Morocco mwishoni mwa Agosti 2019.

Alifika utepeni akiwa wa kwanza baada ya muda wa dakika 15:33.63.

Mshindi huyu wa nishani ya shaba katika mbio za Nyika Duniani mnamo 2017 aliwaonyesha vumbi Waethiopia Feysa Hawi na Tariku Alemitu walioandikisha muda wa dakika 15:33.99 na 15:37.15 mtawalia.

Chelimo alitawazwa malkia wa Afrika katika mbio hizo jijini Brazzaville, Congo mnamo 2015.

Katika mbio nyinginezo za leo Jumatano, Faith Chepng’etich Kipyegon na Winnie Chebet wataelekezewa macho ya karibu watakaposhuka mchujoni kwa nia ya kunyakulia Kenya medali katika kivumbi cha mita 1,500 kwa upande wa wanawake.

Chepng’etich atakuwa akilenga kutetea taji ambalo alilizoa mnamo 2017 Riadha za Dunia zilipoandaliwa jijini London, Uingereza.

Chepng’etich alitawazwa bingwa wa Riadha za Diamond League mnamo 2017 baada ya kushinda fainali jijini Brussels, Ubelgiji na kutuzwa kombe la almasi na Sh5.5 milioni. Alikosa taji la Diamond League mnamo 2016 alipomaliza fainali katika nafasi ya saba na kupoteza tuzo ya Sh4.5 milioni.

Mnamo 2017, Chepng’etich alimduwaza kwa mara nyingine mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za mita 1,500 upande wa wanawake, Genzebe Dibaba wa Ethiopia na kutwaa medali ya dhahabu jijini London.

Chepng’etich ambaye aliibuka bingwa wa Jumuiya ya Madola mnamo 2014, pia alijitwalia medali ya dhahabu katika mbio hizo za mizunguko mitatu katika mashindano ya Olimpiki ya 2016 yaliyofanyika jijini Rio, Brazil.

Chepng’etich ndiye mtimkaji wa pekee aliyeaminiwa kuyabeba matumaini yote ya Kenya ya kupata medali katika mbio hizo za wanawake baada ya wenzake waliopigiwa upatu wa kutamba, Winny Chebet na Judy Kiyeng kubanduliwa mapema.

Aliwapiku kwa urahisi washindani wake wengine wakuu katika mzunguko wa mwisho, wakiwemo Laura Muir (4: 02.97, Uingereza), Sifan Hassan (4: 03.34, Uholanzi) na Laura Weightman (4:04.11, Uingereza).

Dibaba alilazimika kuridhika na nafasi ya 12 kwa muda wa dakika 4:06.72. Simpson ambaye aliishindia USA medali ya pili kabisa katika mbio hizo baada ya kutwaa shaba katika Olimpiki za 2016 jijini Rio, Brazil aliongeza kasi ikiwa imesalia mizunguko miwili na kuwapiku Laura na Caster Semenya wa Afrika Kusini ambaye alipigiwa upatu kutia kapuni nishani ya dhahabu.

Laura Weightman ambaye ni mshikilizi wa rekodi ya mbio hizo katika taifa lake la Uingereza alizidiwa maarifa na kuambulia nafasi ya sita kwa kutumia dakika 4: 04.11.

RATIBA YA (Leo Jumatano):

17:35 Mchujo wa mbio za mita 1,500 wanawake

18:25 Mchujo wa mbio za mita 5,000 wanawake

(Alhamisi):

22:00 Mchujo wa mbio za mita 1,500 wanaume

23:00 Nusu-fainali mbio za mita 1,500 wanawake