Michezo

Matumaini kwa nyota 3 mchujo wa mita 1500 leo Alhamisi

October 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

TIMOTHY Cheruiyot, George Manangoi na Ronald Kwemoi watabeba matumaini ya Kenya ya kujizolea medali zaidi katika Riadha za Dunia watakaposhuka leo Alhamisi ulingoni mwa mchujo wa mbio za mita 1,500 kwa upande wa wanaume jijini Doha, Qatar.

Watatu hao walisalia kuwa tegemeo la pekee la Kenya baada ya bingwa wa dunia aliyetarajiwa kutetea ufalme wake, Elijah Manangoi kujiondoa katika kikosi cha Kenya siku chache kabla ya kuelekea Qatar. Elijah ni kaka mkubwa wa George.

Kwemoi, 24, atapania kuboresha zaidi muda wa dakika 3:28.81 aliouweka katika mbio za Herculis jijini Monaco, Ufaransa mnamo Julai 18, 2014. Ndiye aliyeibuka mshindi wa nishani ya fedha katika Mbio za Nyika za Dunia mnamo 2013 nchini Poland.

George, 20, ndiye aliyeibuka mshindi wa mbio za mita 1,500 wakati wa Michezo ya Afrika (AAG) iliyoandaliwa jijini Rabat, Morocco mwaka huu. Anajivunia pia muda bora wa dakika 3:31.49 aliousajili jijini Monaco, Ufaransa mnamo Julai 12, 2019.

Kujiondoa kwa Elijah, 26, kulichochewa na jeraha la goti ambalo limekuwa likimsumbua kwa muda mrefu msimu huu. Ingawa Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) lilitarajiwa kulijaza pengo la Elijah, mwenyekiti wa AK Tawi la Nairobi, Barnabas Korir alisema jambo hilo lisingewezekana.

Kulingana naye, Elijah alikuwa amepata tiketi ya moja kwa moja ya kupeperusha bendera ya taifa nchini Qatar kutokana na ushindi uliomvunia nishani ya dhahabu katika Riadha za Dunia zilizoandaliwa jijini London, Uingereza mnamo 2017.

Wakati wa riadha hizo za 2017, Elijah alimduwaza bingwa mara tatu wa dunia katika mbio za mita 1,500 Asbel Kiprop na kutia kapuni medali ya dhahabu baada ya muda wa dakika 3:33.61.

Ni ufanisi uliochangia Kenya iliyojizolea jumla ya nishani tano za dhahabu mwaka huo kukamilisha kivumbi hicho katika nafasi ya pili duniani nyuma ya Amerika.

Wajinoa pamoja

George na Cheruiyot ambaye aliambulia nafasi ya pili katika Riadha za Dunia za 2017, wamekuwa wakijinoa pamoja kwa kipindi kirefu mwaka huu hata kabla ya kikosi cha Kenya kuingia kambini kwa minajili ya kivumbi cha Qatar.

Cheruiyot alijikatia tiketi ya kuwakilisha Kenya jijini Doha baada ya kuhifadhi taji la IAAF Diamond League jijini Brussels, Ubelgiji mwishoni mwa Agosti 2019.

Ameridhisha pakubwa katika kampeni za msimu huu ambao ulimshuhudia akinyakua mataji ya duru za Stockholm nchini Uswidi, Stanford nchini Marekani, Lausanne nchini Uswizi, Monaco nchini Ufaransa na fainali jijini Brussels.