Habari

Watu 13 wafariki baada ya basi kugongana na gari jingine eneo la Pala

October 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na BENSON MATHEKA

WATU 13 walikufa Alhamisi usiku basi walimosafiria lilipogogana na trela eneo la Pala, umbali wa kilomita tatu kutoka kituo cha kibiashara cha Awasi, Kaunti ya Kisumu.

Inasemekana basi hilo la kampuni ya Eldoret Express lilikuwa limetoka Uyoma kuelekea Nairobi ajali ilipotokea.

Mkuu wa polisi eneo la Nyanza Vincent Makokha alisema ajali ilitokea kwenye barabara ya Kisumu-Ahero-Nairobi.

“Lori lilikuwa likitoka Eldoret kuelekea Kisumu na kufikia sasa, tumepoteza watu 13,” alisema

Kamanda wa polisi kaunti ya Kisumu Benson Maweu alithibitisha kuwa kati ya watu 13 walikufa kwenye ajali hiyo, 12 walikuwa kwenye basi na mwingine ni dereva wa trela hilo.

Ingawa polisi walisema ajali ilitokea mwendo wa saa saba unusu usiku, duru zilisema kuwa ilitokea mwendo wa saa tano na nusu usiku wa Alhamisi.

Kulingana na kondakta wa basi hili Peter Kamande, ni abiria 36 waliokuwa kwenye basi hilo ajali ilopotokea.

Bw Kamande na manusura wengine wanatibiwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga mjini Kisumu.

Mmoja wa manusura hao, Erickson Muli, ambaye ni afisa wa polisi katika kituo cha Arram, Rarieda alisema alipanda basi hilo katika kituo cha kibiashara cha Ndori.

Abiria mwingine, Bi Caroline Odhiambo aliyekuwa akitoka Asembo kuelekea Machakos alimpoteza mwanawe aliyekuwa na umri wa miaka miwili.

Hata hivyo, mwingine mwenye umri wa miaka sita alinusurika.

Basi lilibururwa na kupelekwa kituo cha polisi cha Awasi.