• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 6:50 AM
LEO VIPI? Kenya uwanjani leo Ijumaa kutetea hadhi ya mbio za viunzi

LEO VIPI? Kenya uwanjani leo Ijumaa kutetea hadhi ya mbio za viunzi

Na GEOFFREY ANENE

REKODI safi ya wanaume wa Kenya katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji katika makala ya 17 ya Riadha za Dunia itakuwa hatarini leo Ijumaa jijini Doha, Qatar.

Kenya, ambayo itawakilishwa na Conseslus Kipruto, Leonard Bett, Abraham Kibiwot na Benjamin Kigen, imetawala makala 14 yaliyopita isipokuwa mwaka 2003 na 2005 ilipopoteza ubingwa kwa mzawa wa Kenya, Saif Saaeed Shaheen, ambaye ni raia wa Qatar.

Hata hivyo, tangu mwaka 2007 Wakenya pekee ndio wamethibitisha hawana kifani katika kitengo hiki ambacho wakimbiaji huruka viunzi 28 na maji mara saba.

Kipruto, ambaye ni bingwa wa Olimpiki, Dunia, Jumuiya ya Madola na Afrika, na mshindi wa michezo ya Afrika, Kigen walipata tiketi za kushiriki fainali kutoka mchujo wa tatu uliokuwa na kasi ya chini kuliko michujo miwili ya kwanza iliyotawaliwa na Waethiopia Getnet Wale na Lamecha Girma. Bett na Kibiwot walimaliza michujo hiyo katika nafasi ya tatu.

Hii inatoa picha kuwa watimkaji hawa wa Kenya watalazimika kumakinika zaidi ili kuendeleza alichoanzisha Moses Kiptanui katika makala ya tatu mwaka 1991.

Mbali na Ethiopia, ushindani mkali kwa Wakenya unaonekana utatoka kwa watimkaji kutoka Marekani, Canada, Uhispania, Ufaransa na Morocco.

Baada ya kuachwa hoi katika mbio za mita 800, Emmanuel Korir naye atatumai kufuta machozi kwa kuwa mmoja wa wanamedali katika mbio za mita 400, leo Ijumaa.

Korir, ambaye alishinda Riadha za Diamond League mwaka 2018 katika kitengo cha mbio za mita 800, alifuzu kushiriki fainali ya mbio za mzunguko mmoja mnamo Jumatano.

Alishinda mchujo wake wa robo-fainali kwa sekunde 45.08 mnamo Oktoba 1 kabla ya kuimarisha muda wake hadi 44.37 akijikatia tiketi ya kushiriki fainali kutoka mchujo wa kwanza ulioshuhudia Mwamerika Fred Kerley akitamba kwa sekunde 44.25. Mkenya mwingine Alphas Kishoyian alibanduliwa nje katika nusu-fainali. Korir atakuwa na kibarua kigumu dhidi ya wakimbiaji kutoka Jamaica, Bahamas, Marekani, Trinidad & Tobago, Grenada na Colombia. Akipata medali ya dunia katika mbio za mita 400, Korir atakuwa Mkenya wa pili kufanya hivyo baada ya Samson Kitur, ambaye ni mwendazake, mwaka 1993.

Matembezi

Kenya pia itakuwa mawindoni katika matembezi ya kilomita 20 ya wanaume ambapo itawakilishwa na Samuel Gathimba.

Bingwa huyu wa Afrika mwaka 2016 na 2018 atalenga kufanya kile Wakenya David Kimutai na Julius Sawe walijaribu bila mafanikio.

Sawe alishiriki makala ya mwaka 2003, lakini akaondolewa kwa kutofuata kanuni za fani hii ambayo si matembezi ya kawaida.

Naye Kimutai alikamilisha katika nafasi ya 31 mwaka 2009 na katika nafasi ya 26 mwaka 2011.

Tukiingia katika siku ya saba ya mashindano hapo jana Alhamisi, Kenya ilikuwa katika nafasi ya tatu nyuma ya Amerika na China kwa medali mbili za dhahabu na mbili za shaba.

Ilivuna dhahabu kupitia kwa Beatrice Chepkoech (mita 3,000 kuruka viunzi na maji) na Ruth Chepng’etich (marathon) nao Ferguson Rotich (mita 800) na Agnes Tirop (mita 10,000) wakazoa shaba.

You can share this post!

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Umuhimu wa kutoa sadaka kwa ajili ya...

Liverpool na Chelsea zajinyanyua Uefa

adminleo