Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Viambajengo muhimu katika utamaduni wa Waswahili

October 4th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

KATIKA makala iliyopita, tulitanguliza mada kuhusu utamaduni ambapo tulipambanua na kutathmini kwa kina vipengele muhimu ikiwemo dhana ya utamaduni na viambajengo muhimu katika utamaduni wa Kiswahili.

Hii leo tutaendeleza mada hii kwa kuangazia viambajengo kadha wa kadha kuhusiana na utamaduni wa Kiswahili.

Ushirikina

Baadhi ya wasomi wanautaja ushirikina kama itikadi. Kwa mujibu wa Mbaabu, ushirikina au itikadi si jambo la Uswahilini tu au linalohusu Waswahili pekee bali ni binadamu wote hata Wazungu, si la Waislamu tu bali ni la Wakristo pia.

Ni muhimu kufahamu kwamba katika jamii zote za binadamu, Itikadi ni taasisi iliyo hai. Aidha, ushirikina ni sehemu ndogo katika itikadi za watu.

Aidha, tunapaswa kuelewa kwamba dini za Kiislamu na Kikristo hazifunzi wala kuhimiza itikadi hii. Hata hivyo, baadhi ya waumini hujikuta wamejitosa wazima wazima katika tasnia hii ya maisha.

Viumbe wa kidhahania

Baadhi ya mambo yanayopatikana katika Itikadi za Waswahili wa mwambao wa Kenya ni pamoja na imani ya kuwepo viumbe wa kidhahania kama vile pepo, majini, mashetani na kadhalika.

Wanajamii huamini nguvu na uwezo wa pepo hao katika kujilinda pamoja na familia zao kutokana na mikosi, nuksi na mikasa.

Vilevile wanaamini uwezo wa pepo hao katika kulinda mali yao kama vile ardhi, mazao, mifugo kusaidia kutibu maradhi, na hata kutumia mizuka na mashetani katika upigaji ramli na kuroga. Itikadi hizi zimeshamiri katika upwa wote wa Waswahili.

Mila na Miiko

Kiambajengo nyeti kingine katika jamii ya Waswahili na Afrika kwa jumla ni kuhusu mila na miiko mbalimbali. Miiko inaweza kufafanuliwa kwa ufupi kama imani maalum za wanajamii zinazofaa kufuatwa na kila mwanajamii ambapo zikikiukwa huweza kuwa na matokeo hatari kama vile majanga au hata kifo kwa mhusika.

Miiko hutumika kukuza maadili mema katika jamii kama vile ukarimu, uaminifu, heshima, ujasiri na kadhalika na wakati uo huo, kuonya dhidi ya ukosefu wa maadili katika jamii kamavile udanganyifu, uchoyo, ukaidi na machukizo mengineyo.

 

[email protected]

Marejeo

Chiraghdin S. (1974). Kiswahili na Wenyewe. Kiswahili 44:1, kur. 48-53.

Chum H. Utamaduni wa Watu wa Wilaya ya Kusini-Unguja. (Mswada unaotayarishwa kutolewa kitabu, Mhariri Dkt. T.S.Y. Sengo).

Mbaabu I. (Mhar.) (1985). Utamaduni wa Waswahili. Nairobi: Kenya Publishing & Book Marketing Co. Ltd