Kipruto ashinda dhahabu mbio za mita 3000 kuruka viunzi na vidimbwi vya maji
Na JAMES MWAMBA na CHARLES WASONGA
ANAYESHIKILIA rekodi ya dunia katika mbio ya mita 3000 kuruka viunzi na maji (steeplechase) Conseslus Kipruto alidumisha ubabe wake Ijumaa kwa kushinda dhahabu katika Mashindano ya Riadha yanayoendelea Doha, Qatar kwa kumshinda raia wa Ethiopia Lamecha Girma utepeni.
Kipruto alishinda kwa kuandikisha dakika 8:01.35 akifuatwa kwa karibu zaidi na Girma aliyemaliza kwa muda wa dakika 8:01:36.
Bingwa wa Afrika katika mbio hizo mnamo 2014 Soufiane El Bakkali kutoka Morocco, ambaye pia alimaliza wa nne katika Mashindano ya Olimpiki ya 2016, naye alikuwa wa tatu kwa kufika utepeni baada ya dakika 8:03.76 na kupata medali ya shaba.
Wakenya wengine walioshiriki mbio hizo ni bingwa wa Mashindano ya Afrika Benjamin Kigen aliyemaliza wa sita kwa dakika 8:06.95, Abraham Kibiwot (8:10.64) aliyemaliza wa saba na mshindi wa medali ya fedha katika Mashandano ya Dunia ya wanariadhi walio na umri wa chini ya miaka 20 Lenaed Kipkemoi Bett (8:1064) aliyetinga nambari tisa.
Kipruto alichomoka kwa nguvu mita chache ziliposalia na ndipo akamlemea Girma mwenye umri wa miaka 18.
Akiongea na wanahabari baada ya ushindi huo, Kipruto alisema Wakenya wengi waliokuwa wakimshangilia katika uwanja huo wa Khalifa jijini Doha ndio walimpa shime na nguvu ya kutoka nyuma ya Girma na kuibuka mshindi.
“Nilipowasikia Wakenya wakiimba na kutushangilia uwanjani, ndipo nikapata nguvu mara moja na kumfuata Girma katika laini ya mwisho. Nilisema singetaka kuwavunja moyo. Kwa hivyo, dhahabu hii ni kwa heshima yao,” Kipruto akasema.
“Ilikuwa ni mbio ngumu. Waethipia (Girma na Getnet Wale) walijua ningelemea mapema na ndipo wakashirikiana kunidhibiti,” akaongeza.
Kipruto anasema kwamba sasa ataelekeza juhudi zake zote katika Mashindano ya Olimpiki mwaka 2020.