Habari

Serikali yatii Raila

October 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MISHI GONGO na DPPS

SERIKALI inajitahidi kutekeleza amri iliyotolewa Jumamosi na Kiongozi wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga kwamba uchimbaji wa mchanga katika Bahari Hindi usitishwe mara moja ili kurahisisha shughuli ya uopoaji wa miili ya Bi Mariam Kighenda na mwanawe Amanda Mutheu.

Msemaji wa serikali, Bw Cyrus Oguna alisema Jumapili uchimbaji wa mchanga baharini bado unaendelea lakini serikali ilikuwa tayari imeanzisha mashauriano na kampuni ya Kichina inayofanya uchimbaji.

Hayo yalijiri huku wanasiasa wa mrengo wa ‘Tangatanga’ wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto, wakitaka watumishi wa umma kupuuza maagizo ya Bw Odinga.

Uchimbaji huo wa mchanga baharini umekuwa ukifanywa kwa miezi kadhaa sasa na kampuni hiyo iliyoletwa na Halmashauri ya Bandari za Kenya (KPA) kwa maandalizi ya ujenzi wa kiegesho cha pili bandarini.

Bw Odinga alisema uchimbaji huo unawatatiza wale wanaoendeleza shughuli za uopoaji, kwani unafanya iwe vigumu kwao kuona vyema chini baharini.

“Serikali bado inaendeleza majadiliano na shirika la Kichina linaloendeleza uchimbaji huo wa mchanga baharini. Matumaini yetu ni kuwa wataafikiana kusimamisha shughuli hiyo, ili kuwezesha wapiga-mbizi kutafuta miili bila tatizo la tope linalojaa kutokana na shughuli hiyo,” alisema Bw Oguna.

Haijafahamika wazi Bw Odinga alikuwa akitoa agizo hilo akiwa na mamlaka gani serikalini, ingawa yeye ndiye Balozi wa Miundomsingi katika Muungano wa Afrika na hivyo basi ana usemi kwa masuala yanayohusu uchukuzi salama wa feri na shughuli za bandarini.

“Tumeambiwa kuwa kuna uchimbaji mchanga unaoendelea hapa karibu na unatatiza uopoaji. Nataka kuagiza hapa kwamba uchimbaji mchanga usitishwe mara moja ili waopoaji waendeleze shughuli zao bila kutatizwa na uchafu unaofanya iwe vigumu kwao kuona chini ya bahari,” alisema Bw Odinga mnamo Jumamosi.

Hata hivyo, wanasiasa wa Jubilee waliokuwa wameandamana na Bw Ruto kwa ibada Jumapili kanisani katika Kaunti ya Meru, walisema Bw Odinga hana mamlaka yoyote kuamrisha serikali.

Viongozi hao walisema anatumia vibaya nafasi aliyopata katika mwafaka wake na Rais Uhuru Kenyatta kujitwika mamlaka asiyokuwa nayo.

“Maagizo hayo ni mzaha wake mwenyewe. Tunaomba watumishi wote wa umma wampuuze. Hana mamlaka aina hiyo,” akasema Mbunge wa Mathira, Bw Rigathi Gachagua.

Wengine waliokuwepo ni Raheem Dawood (Imenti Kaskazini), Moses Kirimi (Imenti ya Kati), Mugambi Rindikiri (Buuri), Silvanus Osoro (Mugirango Kusini) and Mbunge Maalumu Halima Mucheke.

Wakati huo huo, vikosi viwili vya wapigambizi wa kibinafsi kutoka Afrika Kusini vinatarajiwa nchini leo ili kushirikiana na waopoaji wengine kujaribu kutoa miili ya Bi Kighenda na binti yake waliotumbukia baharini katika kivuko cha Likoni wiki iliyopita.

Wataalamu

Shughuli ya uopoaji inaendelezwa na shirika la utoaji huduma za feri (KFS), mamlaka ya bandari (KPA), kikosi maalum cha ulinzi baharini (KCGS) na taasisi ya utafiti wa baharini.

Bw Oguna alisema kikosi cha kwanza kilitarajiwa kuwasili nchini Jumapili jioni huku cha pili kikitarajiwa leo Jumatatu.

Wataalamu hao wanatarajiwa kuharakisha uopoaji.

Kwa upande mwingine, Kanali wa kikosi cha jeshi la wanamaji Lawrence Gituma alisema serikali sasa imeagiza kamera zenye uwezo mkuu wa kuona na kupiga picha sehemu za vina virefu na giza totoro baharini.

Bw Gituma alieleza vifaa hivyo vinavyoendeshwa na remoti, vitatumika badala ya wapiga mbizi kutambua sehemu halisi lilipo gari lililotumbukia majini.

Awali Bw Oguna alisema wamepiga hatua kubwa katika operesheni hiyo, akidai kuwa kati ya sehemu 14 walizotambua kuwa na uwezekano wa kuwa na gari la wendazao, wamebakisha sehemu nne pekee ambazo zina vina virefu mno. Alisema wapiga-mbizi watachukua muda mrefu mno kumaliza sehemu hizo kufuatia vina virefu na hatari ya kukosa pumzi.

“Kuna miili miwili hapo ndani na hatutataka kuongeza mili zaidi, kwa hivyo lazima tujaribu kuangalia usalama wa wapiga-mbizi,” alisema.

Bw Oguna aliwaomba Wakenya na familia ya mwendazake kuwa na subira wanapongojea kukamilika kwa shughuli ya kutafuta miili.