Michezo

City Stars yazidi kutetemesha ligi ya NSL, Ushuru yaangamiza Shabana FC

October 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN KIMWERE

WANASOKA wa Nairobi City Stars waliendelea kufyeka wapinzani wao katika kampeni za kipute cha Supa Ligi ya Taifa (NSL) baada ya kusajili magoli 3-2 dhidi ya Kenya Police kwenye mechi iliyopigiwa uwanjani Karuturi Sports.

Kikosi hicho kimeweka mwanya wa alama nne kati yacho na Bidco United iliyolazwa goli 1-0 na St Josephs Youth lililofungwa na Daniel Kamau.

Nayo Ushuru FC ilizoa ufanisi wa mabao 2-0 mbele ya Shabana FC na kubandua Nairobi Stima katika nafasi ya tatu iliponyoroshwa goli 1-0 Migori Youth.

Dakika ya 15, Arvine Odoyo alicheka na wavu na kuweika Kenya Police kifua mbele kabla ya City Stars kusawazisha kupitia Anthony Kimani dakika sita baadaye. Nao Ebrima Sanneh na Salim ‘Shittu’ Abdalla walibeba City Stars kufanya kweli baada ya kila mmoja kujaza kimiani bao moja dakika ya dakika ya 40 na 74 mtawalia.

Police FC ilijiongezea bao la pili dakika ya 78 kupitia James Gachoka.

Nayo Vihiga Bullets ilitandika Kibera Black Stars (KBS) magoli 3-1 kupitia juhudi zake Levis Baraza, Edwin Wamalwa na Jackson Oketch baada ya kila mmoja kuitingia goli moja.

Hata hivyo, Peter Onduso aliibuka mchezaji bora upande wa KBS alipoifungia bao la kufuta machozi.

Nao washiriki wapya, Northern Wanderers iliendelea kupata mtihani mgumu kwenye kampeni za kinyang’anyiro hicho ilipokubali kucharazwa magoli 3-0 na Murang’a Seal, APs Bomet ilitoka sare ya goli 1-1 dhidi ya FC Talanta huku Mt Kenya United ikiangukia pua ilipofungwa bao 1-0 na Fortune Sacco.

Katika msimamo wa ngarambe hiyo Nairobi City Stars ingali kidedea kwa kufikisha alama 19, nne mbele Bidco United sawa na Ushuru FC tofauti ikiwa idadi ya mabao.