Habari

Ushahidi waanikwa mahakamani jinsi wakili Willie Kimani alivyouawa kinyama

October 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na RICHARD MUNGUTI

SIO siri tena wakili Willy Kimani aliuawa kinyama na polisi, haya ni kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani jijini Nairobi.

Alinyongwa kwa kamba, maiti yake ikatiwa ndani ya gunia na kuvishwa kichwani mfuko wa nailoni wa chapa ya supamaketi ya Mulley ndipo uoze haraka.

Mteja wake Josphat Mwenda na dereva wa teksi Joseph Muiruri pia walitendewa unyama huo – kama wakili huyo – kisha maiti za hao watatu zikatupwa mtoni Athi River eneo la Donyo Sabuk isombwe na maji lakini ikaelea.

Watatu hao walitekwa nyara na Inspekta Leliman na Sajini Leonard Maina Mwangi wakitoka mahakama ya Mavoko na kuzuiliwa kwa muda wa masaa tisa kabla ya kutolewa usiku na “kupelekwa kichinjioni.”

Imefichuka Jumatatu katika Mahakama Kuu kwamba Kachero Peter Ngugi Kamau alilipwa tu Sh2,000 kuwavizia na kuwasaliti watatu hao na polisi walizozana na kutofautiana vikali jinsi ya kutekeleza mauaji hayo.

Hatimaye mwendo wa saa kumi usiku wa manane alinunuliwa chakula na pombe akalewa chakari.

Baadhi yao walitaka Kimani na wenzake waachiliwe kwa vile “maisha yao (polisi) yalikuwa hatarini.”

“Inspekta Leliman alikataa wakiachiliwa na kusema ‘Lazima wafe leo’. Tulikutwa na afisa wa polisi kutoka kituo cha Mlololongo tukizozana ikiwa kimani ataachiliwa au watauawa.Alituuliza kile tunafanya kisha Kamenchu akamweleza wao ni polisi na wako kazi rasmi.Alienda zake.Alikuwa anaendesha gari la Probox. Baada ya kuondoka tu Willy Kimani alitolewa ndani ya buti la gari na kunyongwa na mwili wake kupakiwa ndani ya gunia na kufishwa mfuko wa nailoni wa Supa ya Mulley na kuwekwa ndani ya gari la Leliman.”

Lakini kitendo hicho kilikemewa na afisa msimamizi wa kituo cha Polisi cha Mlolongo aliyemweleza Kamau, “Ona upumbavu wa Inspekta Leliman na Sajini Leonard Maina Mwangi. Wamekamatwa kwa kuua na hawakunieleza walichokitenda. Sasa wako taabani.”

Kachero Kamau alifyata ulimi na hakumweleza OCS kwamba alijua chochote kuhusu mauaji hayo.

Jaji Jessie Lesiit alifahamishwa kwamba maafisa watano wa polisi walihusika katika mauaji ya kinyama ya Kimani, Josphat Mwenda na Joseph Muiruri usiku wa Juni 23, 2016, katika eneo la Mlolongo, Kaunti ya Machakos.

Jaji Lesiit aliambiwa watatu hao Kimani, Mwenda na Muiruri walikuwa wanatolewa kwa buti la gari la Inspekta Fredick Leliman kunyongwa kwa kamba kisha kutiwa ndani ya magunia na vichwa kufungwa mfuko wa nailoni wenye chapa cha Duka la Supa la Mulley.

Watatu hao walinyongwa mmoja baada ya mwingine.

“Watatu hawa walinyongwa kwa zamu na Leliman, Sajini Leonard Maina Mwangi na Kamenchu.Baada ya kutolewa uhai walikuwa walitiwa kila mmoja ndani ya gunia na kufungwa vichwa kwa karatasi ya nailoni. Willy Kimani ndiye alikuwa wa kwanza kuuawa. Alitolewa ndani ya buti la gari la Insp Leliman. Alinyongwa kwa kamba na kichwa kufungwa kwa karatasi ya nailoni kisha akatiwa ndani ya gunia,” Inspekta Geoffrey Kinyua aliambia Jaji Lesiit.

Alisema Mwenda ambaye alikuwa mrefu ndiye alikuwa wa pili kunyongwa jinsi Kimani alivyonyongwa.

“Kwa vile Mwenda alikuwa mrefu, hangetoshea ndani ya gunia moja. Magunia mawili yalitumika; moja kuanzia miguuni na lingine kichwani kisha yakaunganishwa kiunoni kwa kushonwa. Alitiwa ndani ya gari la Kamenchu,” akasema.

Kamenchu hajawahi kukamatwa. Yamkini alitoroka.

Akisoma taarifa ya maungamo ya mmoja wa washtakiwa watano wanaokabiliwa na mashtaka ya kuwaua watatu hao, Kimani, Mwenda na Muiruri, Kachero Peter Ngugi Kamau alisimulia kwa undani jinsi mauaji hayo yalivyotekelezwa.

Kamau alisema ndiye aliagizwa na Inspekta Leliman awavizie na kumwandama Kimani “aliyetakiwa kuuawa kwa kutisha kazi ya Leliman.”

Awasili Mlolongo

Mahakama iliambiwa Kamau alipewa simu ya kuwasiliana na Leliman na mnamo Juni 23, 2016, alifika eneo la Mlolongo saa moja na nusu asubuhi kisha akapatana na Leliman.

Leliman alikuwa na mwanamke ndani ya gari lake aliyeagizwa amtambue Kimani kwa Kamau.

Leliman alikuwa anamtambua Kimani kwa kumtaja kuwa “mtu wa nyama ndogo.”

“Kimani alitambuliwa kwa Kamau na mwanamke aliyekuwa ndani ya gari la Leliman wakiwa Mlolongo asubuhi ya Juni 23, 2016,” alisema Inspekta Kinyua.

Leliman aliyekuwa akiendesha gari lake alikuwa akivizia nje ya mahakama ya Mavoko.

“Kamau alimpigia simu Leliman na kumweleza Kimani na watu wengine wawili walitoka wakiwa ndani ya gari,” Inspekta Kinyua alisema.

Lelimani alimweleza kwamba watatu hao “watauawa wote.”

Mahakama iliambiwa Kimani, Mwenda na Muiruri walisimamishwa katika kivuko cha reli Athi River na kuhamishwa kutoka kwa gari lao na kuingizwa ndani ya gari la Leliman.

Gari lao liliendeshwa hadi Limuru na kuachwa hapo na Kachero Kamau. Alikuwa ameamriwa aliendeshe gari hilo la teksi hadi Meru lakini akaogopa kupitia Zimmerman kwa vile Muiruri alikuwa anahudumu huko na huenda “lingeonekana na wenzake likiwa linaendeshwa na mtu mwingine (Kamau).

Alisema alizima simu tano za wahanga zilizokuwa zimeachwa ndani ya gari hilo la teksi.

Watatu hao walizuiliwa katika kituo cha polisi wa utala wa cha Mlolongo ambapo walitolewa usiku na kuuawa na maiti zao zikapelekwa kutupwa mto Athi River eneo la Donyo Sabuk.

“Kamenchu ndiye aliongoza na kuonyesha eneo la kutupa maiti hizo,” aliungama Kamau.

Alisema: “Leliman na Sajini Leonard Maina Mwangi ndio walikuwa wanatoa maiti kwenye buti za gari na kuzitosa mtoni.”

Alisema baada ya kuzitupa mtoni, walirudi Mlolongo saa kumi usiku na kula na kunywa. Leliman alienda nyumbani naye Sajini Mwangi akaenda kulala kwake Mlolongo.

“Kamenchu aliondoka saa 12 asubuhi nami nikalewa hadi saa kumi mchana kisha nikaenda nyumbani nikaa siku mbili kisha nikarudi kwa OCS na sikusikia kama anafahamu nilikuwa nimehusika na mauaji hayo,” akasema.

Maafisa wa polisi wa utawala Leliman, Stephen Cheburet, Sylvia Wanjiku na Mwangi pamoja na Kamau wamekanusha kuwaua Kimani, Mwenda na Muiruri usiku wa Juni 23/24, 2016 katika eneo la Mlolongo.

Kesi inaendelea.