• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 8:55 AM
MASHUJAA: Timu ya Kenya yapewa mapokezi ya aina yake

MASHUJAA: Timu ya Kenya yapewa mapokezi ya aina yake

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya Kenya ilipokelewa kwa shangwe na nderemo kutoka nchini Qatar mnamo Jumatatu alasiri baada ya kumaliza ya pili kati ya mataifa 209 yaliyoshiriki Riadha za Dunia, huku kila mwanariadha akiimba sasa analenga kufanya ndivyo katika michezo ya Olimpiki mwaka 2022.

Mabingwa hawa wa mwaka 2015, ambao walipokelewa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Michezo Amina Mohamed, walizoa medali tano za dhahabu kupitia kwa Ruth Chepng’etich (marathon), Conseslus Kipruto (mita 3,000 kuruka viunzi na maji – wanaume), Beatrice Chepkoech (mita 3,000 kuruka viunzi na maji – wanawake), Hellen Obiri (mita 5,000) na Timothy Cheruiyot (mita 1,500).

Obiri na Conseslus walitetea mataji yao, huku Chepng’etich, Chepkoech na Cheruiyot wakishinda dhahabu kwa mara yao ya kwanza kabisa.

Faith Kiyegon Chepng’etich (mita 1,500) na Margaret Chelimo (mita 5,000) waliridhika na medali za fedha katika vitengo vyao nao Ferguson Rotich (mita 800), Rhonex Kipruto (mita 10,000), Amos Kipruto (marathon) na Agnes Tirop (mita 10,000) wakavuna medali za shaba katika vitengo hivyo.

Mapumziko

Katika mahojiano baada ya kuwasili jijini Nairobi, wengi wa wanariadha waliowakilisha Kenya akiwemo nahodha wa timu hiyo Julius ‘YouTube Man’ Yego, walieleza Taifa Leo kuwa wataingia mapumziko ya mwezi mmoja kabla ya kuanza kujinoa kwa msimu ujao, ambao mashindano makubwa kwenye ratiba ya dunia ni Olimpiki jijini Tokyo nchini Japan.

Aidha, mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji Beatrice Chepkoech alifichua kuwa atavizia rekodi ya Olimpiki ya dakika 8:58.81 inayoshikiliwa na Mrusi Gulnara Galkina tangu mwaka 2008.

Rekodi ya dunia ya Chepkoech ni 8:44.32 aliyotimka mjini Monaco mwaka jana.

Marekani ilishinda mashindano haya yanayofanyika kila baada ya miaka miwili kwa mara yake ya 13 kwa jumla na pili mfululizo.

Iliambulia medali 14 za dhahabu, 11 za fedha na nne za shaba. Jamaica ilifunga mduara wa mataifa tatu-bora kwa dhahabu tatu, fedha tano na shaba nne.

You can share this post!

Rais apuuza uwezekano wa serikali kupinduliwa

De Gea asema Manchester United ya sasa sio kama ya zamani

adminleo