• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 2:25 PM
SHANGAZI AKUJIBU: Alikuwa na nia gani kuniambia tukapimwe?

SHANGAZI AKUJIBU: Alikuwa na nia gani kuniambia tukapimwe?

Na SHANGAZI

HUJAMBO shangazi? Nina umri wa miaka 32 na nina uhusiano na mwanamume ambaye ameoa. Tumekuwa pamoja kwa miaka miwili sasa. Hivi majuzi alinishtua sana aliponiambia kuwa ana virusi na akaniomba twende tukapimwe. Tulienda na tukapatikana tuko sawa. Kufikia sasa sijaelewa alikuwa na nia gani na bado nina wasiwasi. Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Inawezekana kwamba mwanamume huyo alitumia madai hayo kama njia ya kukushawishi mwende mkapimwe. Lakini alifanya makosa kwa sababu hilo silo jambo la kufanyia mzaha. La sivyo, labda ana uhusiano na wanawake wengine na amekuwa akijishuku kwa hivyo alitaka kujua hali yake na yako pia. Kama kawaida, mimi suing mkono mipango ya kando. Naona wewe bado ni mwanamke mchanga na ushauri wangu ni kwamba uachane na mume wa wenyewe utafute wako. Ni kwa kwa njia hiyo pia ambapo utaondoa wasiwasi ulio nao kutokana na kisa hicho.

 

Kakangu katwaa dada ya kidege changu

Kwako shangazi. Nina jambo ambalo naomba unisaidie kutatua. Nina mpenzi ambaye tunapendana kama chanda na pete. Uhusiano wetu umefikia miaka mitano sasa na tunaendelea na mipango ya ndoa. Lakini ghafla ndugu yangu amemnyakua dada ya mpenzi wangu na kumuoa katika muda wa miezi miwili pekee. Hatua yake hiyo imenichanganya, sijui nitafanya nini. Nishauri.

Kupitia SMS

Wasiwasi wako hasa ni kwamba hutaweza kumuoa mpenzi wako kwa sababu tayari ndugu yako amemuoa dada yake. Sina hakika kuhusu iwapo ni makosa ama mwiko kwa ndugu kuoa kutoka familia moja. Hilo ni jambo nadra sana na ninaamini jamii tofauti zina msimamo wake kulihusu. Ushauri wangu ni kwamba uwauliza wazazi wako na jamaa zako wengine naye mpenzi wako afanye hivyo hivyo kwa upande wake ili mjue mwelekeo wa mpango wenu.

 

Namshuku sana mpenzi wangu

Shikamoo shangazi! Mpenzi wangu ambaye tulimaliza pamoja masomo ya chuo kikuu mwaka uliopita amepata kazi katika kampuni fulani. Tangu ajiunge na kampuni hiyo, kuna mwanamume ambaye amekuwa akimpigia simu karibu kila jioni akitoka kazini na wikendi pia. Nimemuuliza mpenzi wangu akaniambia wanafanya kazi pamoja mwanamume huyo. Ninashuku wameanzisha uhusiano wa kimapenzi kwani sioni sababu nyingine ya mwanamume huyo kupiga simu kila siku. Nishauri.

Kupitia SMS

Ni jambo la kawaida kwa watu kubadili maamuzi kuhusu maisha yao. Kwa sababu hiyo, halitakuwa jambo lisilo la kawaida kwa mpenzi wako kuvutiwa na mwanamume mwingine na kuvunja uhusiano wenu. Tabia ya mwanamume huyo ya kumpigia simu kila siku ni dalili kuwa anamtaka. Jambo ambalo huna hakika nalo ni iwapo amekubali ombi lake au la. Kama bado mko pamoja na hajakwambia kuwa amepata mwingine, ushauri wangu ni kuwa uchukulie kwamba hakuna chochote kinachoendelea kati yao kwa sasa. Mambo yakibadilika ni lazima utajua ama yeye mwenyewe akwambie.

 

Nimuoe huyu wa mtoto ama niachane naye?

Shangazi pokea salamu zangu. Nina umri wa miaka 22 na nina mpenzi ambaye anataka nimuoe. Tatizo ni kwamba ana mtoto ambaye alizaa na mwanamume aliyekuwa mpenzi wake na wakaachana. Je, nimuoe ama niachane naye?

Kupitia SMS

Mtoto hawezi kuwa kikwazo cha wawili wakipendana. Nimeshuhudia wanaume wakioa wanawake walio na watoto hata watano. Kama kweli unampenda mwanamke huyo na uko tayari kumuoa, basi mkubali mtoto pia. Ukweli ni kuwa huwezi kumtenganisha na mtoto wake.

You can share this post!

PATA USHAURI WA DKT FLO: Miguu huuma wakati wa baridi,...

Matiang’i awataka viongozi wa kidini kuisaidia...

adminleo