• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 1:51 PM
Nyota wa raga wakubali kurejea katika kikosi cha taifa

Nyota wa raga wakubali kurejea katika kikosi cha taifa

Na CHRIS ADUNGO

WANARAGA wazoefu na wa tajriba pana akiwemo Collins Injera anayejivunia kufunga idadi kubwa zaidi ya trai, wamekubali kurejea katika timu ya taifa ya wachezaji saba kila upande kwa minajili ya kampeni za duru ya Raga ya Dunia ya 2020.

Kurejea kwa nyota hao kunajiri siku chache baada ya Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) kumpokeza mikoba kocha Paul Feeney ambaye ni mzawa wa New Zealand.

Feeney, ambaye kwa sasa atasaidiwa na Kevin Wambua, pia ana kibarua kikubwa cha kuwaongoza Kenya Shujaa kufuzu kwa Olimpiki za 2020 zitakazoandaliwa jijini Tokyo, Japan.

Kwa pamoja na William Ambaka, Oscar Ouma, Samuel Oliech, Billy Odhiambo na Dennis Ombachi, Injera ni sehemu ya kikosi cha wanaraga 24 wa haiba kubwa ambao Feeney amewaita kambini kwa minajili ya kivumbi cha kimataifa cha Safari Sevens kitakachoandaliwa uwanjani RFUEA, Nairobi kati ya Oktoba 18-20, 2019.

Wengine ni Andrew Amonde, Daniel Sikuta, Nelson Oyoo, Eden Agero, Brian Tanga na Dennis Ombachi ambao kwa sasa watashirikiana na chipukizi

Davis Nyaundi (Menengai Oilers), Joel Inzuga na Mike Okello (Mwamba RFC), Monate Akuei (Nakuru RFC) na Ian Mabwa (Nondescripts).

Shadon Munoko, Mark Wandeto, Eliakim Kichoi, Cyprian Kuto na Brian Wahinya ni wanaraga wazoefu ambao Feeney amewatema katika kikosi chake licha ya kuwa sehemu muhimu ya kampeni za Shujaa chini ya mkufunzi Paul Murunga msimu uliopita.

“Tumekifanyia kikosi mabadiliko makubwa. Tunapania sasa kuimarisha zaidi uthabiti wa kila idara na kuhakikisha kwamba kila mchezaji anadumisha ubora wa fomu hadi mwishoni mwa kampeni muhimu zijazo,” akasema Feeney.

Ufalme wa Safari Sevens

Jumla ya vikosi 14 tayari vimethibitisha kunogesha makala ya Safari Sevens mwaka huu wa 2019.

Mbali na Samurai ambao ni mabingwa watetezi, vikosi vingine vitakavyowania ufalme wa taji hilo ni timu za taifa za Afrika Kusini, Uhispania, Zimbabwe, Uganda na Zambia pamoja na Russia Academy, Kenya Morans na KCB ambao ni miamba wa raga ya humu nchini.

Klabu nyinginezo ni Western Province na Blue Bulls za Afrika Kusini, Seventise Rugby ya Ufaransa na wapambe wa raga ya Urusi, Narvskaya Zastava.

Duru za Raga ya Dunia zitaanza rasmi mnamo Novemba jijini Dubai na Kenya iliyoambulia nafasi ya 14 msimu jana itapania kuimarisha matokeo yake.

Kabla ya hapo, Kenya itawania pia tiketi ya Olimpiki za 2020 kwa kushiriki mchujo utakaondaliwa jijini Johannesburg, Afrika Kusini.

Vijana wa Feeney watakuwa na kibarua kizito cha kuwazidi maarifa Zimbabwe, Uganda, Madagascar, Zambia, Tunisia, Senegal, Morocco, Namibia, Ghana, Botswana, Mauritius, Ivory Coast na Nigeria.

You can share this post!

Bale kujiondoa Madrid akipata mwanya

INEOS 1:59 Challenge: Dunia kusimama Eliud Kipchoge...

adminleo