Haji, Kinoti wasifu maaskofu kwa msimamo wao kuhusu ufisadi
Na BENSON MATHEKA
MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji na mwenzake wa Uchunguzi wa Jinai (DCI), George Kinoti, wamepongeza maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini kwa kuchukua hatua ya ‘kupiga vita’ ufisadi kupitia marufuku ya harambee za wanasiasa makanisani.
Kwenye taarifa ya pamoja, wawili hao walisema kwamba hatua ya maaskofu hao ni mwelekeo unaofaa katika vita dhidi ya uporaji wa mali ya umma.
“Tunawapongeza kwa dhati maaskofu hao kwa kuchukua msimamo thabiti na kutoa ushauri wa kiroho ambao unahitajika sana katika vita dhidi ya ufisadi. Hii ni hatua inayopaswa kuigwa,” walisema kwenye taarifa.
Maafisa hao ambao wamekuwa msitari wa mbele katika vita dhidi ya ufisadi na uhalifu wa kiuchumi walisema kwamba walikutana na viongozi wa kidini mwaka 2018 na kuwataka kujiunga nao kufanikisha vita dhidi ya ufisadi.
“Tuliwahimiza wajiunge nasi kwenye vita hivi na leo tunafurahishwa na hatua yao ya kutuunga mkono,” walisema.
Walisema ufisadi hauwezi kuangamizwa kupitia mfumo wa kisheria pekee, mbali pia kupitia mafunzo ya kidini katika jamii.
“Dini ina nguvu katika maisha ya mwanadamu…msimamo wa maaskofu wa kanisa katoliki unatoa nafasi kwa waumini kujipeleleza na kutia nguvu imani yao kwa maadili na uwajibikaji,” walisema.
Kauli ya maaskofu hao Jumamosi iliyopita ilizua mjadala mkali nchini baadhi ya wanasiasa wakiwaunga mkono na wengine kuipinga.
Kulingana na maaskofu hao, wanasiasa wanaotaka kutoa michango kanisani wanapaswa kufanya hivyo kupitia njia inayoweza kubainishwa wanavyopata pesa hizo.
Walipiga marufuku wanasiasa kutoa mabunda ya noti kanisani. Hata hivyo, walisema wanasiasa wamekaribishwa makanisani na kutoa sadaka kama waumini wengine.