BONGO LA BIASHARA: Alipitia mengi kabla kupata kitulizo katika kuuza samani
Na CHRIS ADUNGO
WAFANYABIASHARA wakubwa na wadogo ni mhimili utakaowezesha taifa letu kufikia ruwaza ya mwaka wa 2030.
Ingawa baadhi ya wananchi huchukulia kuwa kazi za ofisi pekee ndizo zinazoweza kumhakikishia mtu maisha bora, ukweli ni kwamba hata kazi nyingi za kujiajiri zinalipa sana.
Bernard Ouma ni mmoja wa Wakenya ambao wamechukua hatua ya kujiajiri na kutegemea kazi zao binafsi ili kupata riziki ya kila siku. Yeye ameungana na wenzake wengine wanne na kukodi sehemu ya kufanyia biashara kutengeneza samani katika mtaa wa Umoja, Embakasi Magharibi, Nairobi.
Ouma mwenye umri wa miaka 36 anasema kwamba kazi hii imetoa ajira kwake na huwa inalisha familia yake na kukimu mahitaji mengine ya kimsingi ya mkewe na watoto wawili.
Kabla ya kuanza kazi hii, alipitia changamoto nyingi maishani kutokana na malipo ya kiwango cha chini alipokuwa akifanya kazi za vibarua kwa miaka minane katika kampuni moja iliyokuwa ikiuza samani nje ya nchi kutoka eneo la Viwandani, Nairobi.
Hali hii ilikuwa ngumu kwake lakini akawa na uvumilivu ili apate tajriba ya kutosha. Kilele cha masaibu yake wakati huo ni pale ambapo kampuni hiyo iliwapa notisi ya kuachishwa kazi baada ya kununua mashine ghali zaidi za kufanya kazi walizokuwa wakizifanya wao kwa mikono.
Hapo ndipo aliamua kwamba ni lazima atafute kazi mbadala. Haukupita muda mwingi kabla ya kupatana na wenzake na kuanza kazi yao wenyewe ya samani katika sehemu kidogo mtaani Umoja kutokana na hela kidogo walizokuwa nazo.
Ouma anaelezea kuwa walijitia moyo katika sehemu hii na walipoanza kuona mafanikio haya, walihamia eneo jingine mtaani mumo humo ambako walipata nyumba kubwa ya kazi.
Kulingana naye, huwa ananunua mbao, vioo na bidhaa nyinginezo na kujiundia vyombo vyake mwenyewe. Kwa sasa kila mmoja anatengeneza bidhaa zake na kuuza kwa wateja wanaojitafutia au wanaojileta katika karakana yao.
Baadhi ya bidhaa anazotengeneza ni pamoja na vitanda, viti, kabati za televisheni, kabati za kuwekea nguo, rafu, meza, viti vya ofisi nk.
Ouma anasema wateja wake mara nyingi ni wapita njia ambao huona bidhaa zake nzuri na kuomba kutengenezewa kama hizo na mara nyingine kununua zizo hizo. Wateja hawa pia wana manufaa kwake kwani huwa wanaelezea marafiki zao na kuwaelekeza kwake.
Zaidi ya hapo, huwa anachapisha picha za bidhaa zake kwenye mitandao na kupata idadi kubwa zaidi ya wateja.
Mara nyingi huwa anapiga picha za bidhaa zake na kuziweka kwenye mtandao mmoja wa uuzaji na ununuzi bidhaa Kenya huku akielezea anapopatikana na nambari ya simu ambayo mteja anaweza kuzungumza naye ili kufanikisha shughuli za uuzaji na ununuzi.
Yeye huzungumza na wateja wake kuhusu bidhaa wanazotaka kununua au kutengenezewa na kuelewana jinsi watakavyotoa malipo na ya kiwango gani.
“Mara nyingi wateja hununua bidhaa kwa pesa taslimu. Wanaoomba kutengenezewa huwa wanatoa kiasi fulani cha malipo ya awali (arbuni) kisha kutoa fedha za ziada baadaye wanapozipokea bidhaa zao,” Ouma anasimulia.
Aidhaa, anasema kuwa siku zijazo anapania kupanua biashara hii na apate nafasi atakapofanyia kazi hii kivyake.
Kazi yampa riziki ya kila siku
Anasema kazi hii inamfaa kwa sasa manake inampa riziki ya kila siku ambayo pia imemwezesha kuwasomesha ndugu zake wadogo katika ngazi za shule ya sekondari na chuo kikuu.
Baadhi ya changamoto ambazo huwa anakumbana nazo ni pamoja na bei ghali ya vifaa anavyohitaji ili kuwaundia wateja samani wanazozihitaji au kuagiza. Hali hii anasema inatokana na hali ngumu ya kiuchumi na kupanda kwa gharama ya maisha. Hili pia humweka katika ulazima wa kuongeza bei ya bidhaa hizi anazojitengenezea ili angalau apate faida.
Changamoto nyingine ni ushindani mkubwa unaotokana na kuwepo kwa biashara nyingi za aina hii. Kulingana naye, hili linapunguza ujira anaoupata kutokana na mauzo kidogo ya kila siku. Pia anasema kuwa gharama ya juu ya kulipia nguvu za umeme ni changamoto kubwa kwani kazi yake nyingi hutegemea kuwepo kwa nguvu za umeme.
Hata hivyo, huwa anajitahidi na kuunda bidhaa zenye ubora wa kipekee.