Hatimaye gari na miili ya mwanamke na bintiye yaondolewa baharini
Na MISHI GONGO
BAADA ya Wakenya kusubiri kwa siku 13, gari lililotumbukia katika Bahari Hindi kutoka feri kwenye kivuko cha Likoni, Kaunti ya Mombasa liliopolewa Ijumaa huku wakazi wakishangilia kwa kukamilishwa kwa shughuli ya kulitafuta.
Japo ilikuwa na huzuni kwa kuwapoteza wapendwa wao, familia ya Bi Mariam Kighenda na binti yake Amanda Mutheu ilipata afueni gari hilo lilipovutwa kutoka chini ya bahari saa kumi na robo Ijumaa alasiri.
Viongozi kadhaa kutoka Kaunti ya Mombasa wakiongozwa na Gavana Hassan Joho na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Sheriff Nassir walifika eneo la mkasa kuungana na familia shughuli hiyo ilipokuwa ikiendelea.
Katibu wa Wizara ya Uchukuzi Esther Koimett na wakuu wa huduma za feri pia walishuhudia shughuli hiyo.
Vioo vya gari hilo la rangi nyeupe havikuwa vimevunjika japo lilikuwa limepondeka sehemu tofauti.
Baada ya miili ya Bi Kighenda na mwanawe kuopolewa, maombi yaliandaliwa na kikosi cha jeshi la wanamaji kabla ya kupelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya Jocham.
Viongozi wa Kikristo wakijumuisha wa Kanisa Katoliki na lile la Angilikana waliombea familia ya marehemu Mungu awafariji kwa kupoteza wapendwa wao.
“Hii ni desturi ya jeshi la wanamaji,” alisema msemaji wa serikali Cyrus Oguna.
Baada ya maombi, wakuu wa jeshi na serikali waliongoza jamaa na marafiki kuweka maua katika eneo la mkasa.
Familia pia iliruhusiwa kufanya maombi eneo la mkasa.
Msemaji wa familia Luca Mbati alisema kuwa siku ya mazishi itapangwa kulingana na hali ya miili itakavyokuwa.
“Tutaanza mipango ya mazishi na tutakuwa tukikutana Tudor. Taarifa zaidi itatolewa baadaye,” alisema.
Suala la mazishi limezua utata kati ya familia ya mwendazake na mumewe, familia ya mke ikishikilia kuwa mazishi yatafanyika nyumbani kwao kwa kuwa mumewe hakuwa amemlipia mahari huku mumewe kupitia msemaji wa familia akisema mwili utazikwa Kaunti ya Makueni.
Bi Kighenda na bintiye Amanda Mutheu aliyekumbana na mauti akiwa na umri wa miaka minne, walizama Septemba 29, baada ya gari lao aina ya Toyota ISIS lenye nambari ya usajili KCB 289C kuteleza kutoka ndani ya feri ya MV Harambee na kutumbukia ndani ya maji.
Changamoto
Operesheni ya uopoaji iliyoanza Oktoba 1 na kumalizika Oktaba 11 mwenda wa saa kumi na robo mchana ilikumbwa na changamoto kadha wa kadha zikiwemo mawimbi makali, kukosa vifaa na wataalamu na hali mbaya ya hewa.
Shughuli hiyo iliyoongozwa na kikosi cha jeshi la wanamaji wakishirikiana na shirika la utoaji huduma za feri (KFS), mamlaka ya bandari (KPA), kikosi maalum cha ulinzi baharini (KCGS), taasisi ya utafiti wa baharini na kupigwa jeki na wapigambizi kutoka Afrika Kusini.
Jumatano wiki hii msemaji was serikali alisema walipoanza shughuli ya kutafuta miili na gari la mwendazake baharini, walitambua sehemu 14 ambazo walishuku lingekuwa limezama.
“Tumetambua sehemu 14 tukifuatilia moja baada ya nyingine hadi pale tutakapopata gari la mwenda-zake,” alisema.
Jumanne msemaji huyo alisema msako wa kutafuta gari la Bi Kighenda ulikuwa umesalia mita 300 pekee kati ya kilometa 1.2 ambazo kikosi cha uopoaji kilikuwa kimetambua kuwa na uwezekano wa kulipata. Alieleza walifanikiwa kufikia hapo kwa kutumia kifaa maalum kilichonunuliwa na serikali –three beam system– chenye uwezo wa kuona katika sakafu ya bahari kwa kutumia mfumo wa 3D na hivyo kutoa picha halisi.
“Tuna matumaini kuwa sehemu mojawapo kati ya hizi, kutakuwa na uwezekano wa kuwa na gari lililozama kufuatia ishara ya mchanga wa sehemu hiyo umevurugwa na chombo ambacho si cha baharini,” alisema.
Bw Oguna, alisema picha walizopiga katika sehemu walizotambua katika sehemu mbili walizoshuku kuwa na gari, zilionyesha utandu wa tope la mita 1.5 na ishara ya chombo ambacho si kawaida kuwa baharini.