Mvua iliyopitiliza kiwango yaendelea kushuhudiwa katika maeneo mengi nchini

Na FARHIYA HUSSEIN, ALEX NJERU na CHARLES WASONGA

MVUA kubwa itaendelea kushuhudiwa nchini, imesema idara ya utabiri wa hali ya hewa, huku biashara na shughuli za uchukuzi zikiwa zimeathirika pakubwa eneo la Pwani na wakazi wanaoishi katika maeneo yanayoweza kuathirika na mafuriko na maporomoko ya ardhi katika kaunti ya Tharaka Nithi wakishauriwa kuchukua tahadhari kuu.

Hii ni baada ya watabiri wa hali ya hewa kutoa onyo kuwa mvua utaendelea kushuhudiwa pamoja na upepo mkali wiki nzima.

“Maeneo tofauti inatarajiwa yatashuhudia mvua nyakati za asubuhi na jioni. Pia, usiku kunatarajiwa mvua chache,” akasema mkurugenzi wa idara ya hali ya hewa Mombasa, Edward Ngure.

Mvua hiyo ambayo imekuwa ikiendelea imesababisha hasara kubwa; hasa kwa majumba na barabara kadhaa.

Mkazi wa Tudor, Kaunti ya Mombasa, Ole Koyiet amesema walishuhudia ukuta wa jengo ambalo ujenzi wake umekuwa ukiendelea kujengwa, ukianguka kutokana na athari za mvua.

“Tunashukuru Mungu kwani ujenzi haukuwa ukiendelea wakati ukuta huo ulianguka. Wengine walilazimika kutulia ndani ya kanisa mpaka mvua ikapusa,” amesema Bw Koyiet.

Kamishna wa Pwani, John Elungata ametoa onyo kwa wanaoishi katika mitaa ya madongoporomoka kuhamia eneo salama.

“Tumepata taarifa maeneo tofauti tayari wamezingatia mafuriko kwa hivyo naomba watu wawe makini sana na kuchukua tahadhari wasisombwe na mvua hii,” amesema Bw Elungata.

Pia, ofisi husika kwenye serikali zimeshauriwa kujipanga mapema kwani mvua hiyo inaendelea kushuhudiwa.

Aidha, sekta ya usafiri pia imeathiriwa ikiwemo barabara eneo la Likoni, Mvita, Changamwe na Jomvu.

Mwenyekiti wa chama cha matatu nchini, Ali Salim amerai serikali kuu kuziba mashimo yaliyoachwa wazi barabarani ili kupunguza visa vya ajali msimu huu wa mvua.

“Mashimo madogo yaliyo wazi barabarani yamekuwa tishio kwa madereva wetu. Ni muhimu yazibwe na barabara kukarabatiwa ili kupunguza ajali zinazosababishwa na mashimo hayo,” akasema Bw Salim.

Mabaharia na wengine wenye shughuli za baharini wametakiwa kuwa waangalifu zaidi.

Katika Kaunti ya Tharaka Nithi,  watu wanaoishi katika maeneo yanayoweza kuathirika na mafuriko na maporomoko ya ardhi wameshauriwa kutahadhari wakati huu eneo hilo linaposhuhudia mvua kubwa.

Mvua hiyo tayari imeharibu barabara na mimea shambani katika sehemu nyingi katika kaunti hiyo ambayo imekumbwa na kiangazi kwa kipindi kirefu.

Akiongea katika kijiji cha Gaceeraka, kaunti ndogo ya Tharaka Kusini, naibu gavana Nyamu Kagwima alisema wikendi kwamba mvua hiyo huenda ikasababisha uharibifu mkubwa kwa sababu watu walifyeka maeneo chepechepe na kupanda mimea.

“Watu wanapaswa kuwa waangalifu wakati wa mvua kubwa; hasa wale wanaoishi katika maeneo yanayoweza kushuhudia mafuriko ili kuzuia maafa,” akasema Bw Kagwima.

Sasa wakazi wameshauriwa kupanda miti kando ya mito na katika sehemu fulani za mashamba yao kama njia ya kutunza mazingira.

Bw Kagwima alisema serikali ya kaunti inapanga kujenga mabwawa kando ya mito ambayo hukauka nyakati za kiangazi kama njia ya kuhifadhi maji kwa matumizi katika msimu wa kiangazi.

Alisema kuwa katika msimu uliopita wa kiangazi mito yote, hasa katika maeneobunge ya Tharaka na Chuka/Igambang’ombe, ilikauka na kusababisha mahangaiko kwa watu pamoja na mifugo wao.

“Hii ndio maana ni tumewekeza kiasi fulani cha fedha kufadhili ujenzi wa mabwawa kando ya mito yetu,” Bw Kagwima akasema.

Habari zinazohusiana na hii

Maafa ya mvua yasambaa

Maafa zaidi

37 wazikwa hai

Mvua yazua maafa Pwani