Makala

OBARA: Tufadhili wanaspoti badala ya idara hizi zinazosinzia

October 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

MACHO ya mamilioni ya watu ulimwenguni yaliekekezwa kwa Mkenya mmoja ambaye ni Eliud Kipchoge, katika harakati zake za kujaribu kukamilisha mbio za marathon Jumamosi iliyopita ambapo alifaulu kukamilisha chini ya muda wa saa mbili.

Nina hasira kutokana na jinsi kwa mara nyingine, idara zilizopewa jukumu la kutangaza Kenya kimataifa zilivyozubaa na kuacha nafasi mwafaka kupita bila kufanya chochote cha maana.

Serikali hutenga bajeti ya mamilioni ya pesa kila mwaka kwa idara ambazo nyingi zao ziko chini ya Wizara ya Utalii na ile ya Biashara ili kutangaza Kenya kwa nchi za nje kwa nia ya kuvutia watalii na uwekezaji.

Kinachonitia hamaki ni jinsi fedha nyingi na rasilimali hizo zinazotengwa huwa hazitumiwi kwa njia inayofaa.

Utakuta kwamba, kile ambacho hufanywa na maafisa husika waliopewa jukumu hili ni kuandaa warsha za kitaifa na kimataifa katika hoteli za kifahari.

Kando na gharama za maandalizi, fedha nyingi huishia mifukoni mwa watu wachache ambao lazima walipwe marupurupu kuhudhuria warsha hizo na pengine nauli ya ndege na makazi.

Hayo yanapotendeka, kuna raia ambao hawalipwi mishahara yoyote na serikali lakini kupitia kwa talanta zao, wanainua bendera ya Kenya juu kwa fahari kubwa kila wakati wanapojitosa katika kile wanachokienzi.

Wengi wa raia hawa ni wanaspoti wanaojumuisha wanariadha, wachezaji soka, wanandondi, wachezaji voliboli, wale wa raga, waogeleaji miongoni mwa wengine.

Sawa na Kipchoge alivyotuletea fahari wikendi licha ya kufadhiliwa na kampuni ya kibinafsi ambayo hata si ya Kenya bali ya Uingereza, kuna wananchi wengi ambao hukumbukwa na serikali tu baada yao kufana katika nyanja zao tofauti.

Kwa wale ambao hubahatika kupata ufadhili wa serikali, si mara moja wala mbili tumeshuhudia jinsi ufadhili huo hutolewa shingo upande na wengine wao kufurushwa kutoka kwa hoteli ambazo zilihitajika kugharamiwa na serikali.

Ingekuwa bora kama serikali itakoma kuharibu pesa na rasilimali kwa idara ambazo hazitusaidii kivyovyote kutangaza sifa za taifa hili kimataifa ikilinganishwa na jinsi raia hawa wenzetu wanavyofanya.

Hizo idara zimebaki kuwa sehemu za kuwaundia watu wachache walio wandani wa wenye ushawishi serikalini nafasi za ajira wanakoweza kunyonya pesa za umma bila kufaidi taifa.

Ni heri hizo rasilimali zielekezwe kwa idara nyingine kama vile za spoti ili kukuza talanta za vijana wanaoweza kutuletea fahari ugenini, na kufadhili wanaspoti kwa mashindano ya kimataifa.

Hii tabia ya serikali kukaa kitako na kusubiri hadi dakika za mwisho ndipo ianze kutapatapa ikitaka kufaidika kutokana na jasho la raia inafaa ikome, kwani ni aibu inayochukiza sana.

Mwisho, hongera Kipchoge kwa kutuonyesha kwamba, hakuna kisichowezekana kwa binadamu mradi tu ajitolee kikamilifu kukitekeleza!