ADUNGO: KPL na timu zisipotafuta mdhamini mpya ni bayana soka itaathiriwa vibaya nchini
Na CHRIS ADUNGO
MWISHONI mwa wiki jana, kikosi cha Kakamega Homeboyz kiliwataka wasimamizi wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) kusitisha kivumbi hicho kwa muda hadi changamoto za kifedha zinazokabili klabu zinazowania ubingwa wa kipute hicho zitatuliwe.
KPL kwa sasa inapitia panda-shuka tele tangu SportPesa ambao walikuwa wadhamini wa Ligi Kuu wasitishe shughuli zao zote humu nchini. Ombi la Homeboyz la kutaka kivumbi cha KPL kisitishwe liliungwa na klabu sita nyinginezo zinazokabiliwa na ugumu wa kujiendesha na kugharimia mishahara ya wachezaji.
Miongoni mwa klabu hizo ni Chemelil Sugar, Nzoia Sugar, Mathare United, Kariobangi Sharks, Kisumu AllStars na SoNy Sugar iliyokosa kufika uwanjani kwa minajili ya kipute kilichopita cha KPL dhidi ya AFC Leopards.
Baada ya kupigwa kwa mechi za raundi ya nne ya ligi msimu huu, maafisa na marefa waliosimamia michuano hiyo bado hawajalipwa hata peni moja kutoka KPL.
Kujiondoa rasmi kwa kampuni za SportPesa na Betin katika soko la humu nchini kulimaliza mvutano wa muda mrefu kati yazo na Serikali ya Kenya kuhusu kanuni mpya za ushuru.
Pindi baada ya kutoa tangazo hilo, usimamizi wa Betin ulitoa notisi ya kutimuliwa kwa wafanyakazi wao wote kutokana na changamoto za kifedha. Betin walikariri kwamba juhudi za kutafuta suluhisho kati yao na Serikali kati ya Julai na Septemba mwaka huu ziligonga mwamba na hivyo kuwawia vigumu kuwadumisha wafanyakazi wao. Kwa upande wao, vinara wa SportPesa walikiri kutamaushwa na uamuzi wa Serikali wa kutoza ushuru wa hadi asilimia 20 kwa kila ushindi.
Kuvunjika rasmi kwa mahusiano ya Kenya na kampuni hizi za kamari kunatazamiwa kuathiri pakubwa hali na maendeleo ya kabumbu na michezo mingine ya humu nchini.
Mbali na mchango wa karibu Sh700 milioni ambao SportPesa walikuwa wakitoa kila mwaka kwa minajili ya kufanikisha kampeni za Ligi Kuu ya Kenya (KPL) kujiondoa kwa wadhamini hao ni tukio litakalotikisa pakubwa maendeleo ya mchezo huo iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa na wahusika.
Ikumbukwe kwamba hadi walipojiondoa, SportPesa walikuwa pia wakidhamini timu za taifa za raga na voliboli. Kwa kipindi kirefu, KPL wamekuwa wakiwategemea sana SportPesa kugharimia mishahara ya wafanyakazi wao huku mchango wao pia ukisaidia pakubwa klabu 18 zinazoshiriki kampeni za Ligi Kuu.
Kila kikosi kinachowania ubingwa wa KPL kimekuwa na uhakika wa kupokezwa mgao mkubwa kwa mwaka kutoka kwa SportPesa ambao wamekuwa wakifadhili Gor Mahia na AFC Leopards.
Ipo haja kuu basi kwa maafisa wa KPL na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kujitahidi vilivyo kuwarejesha SportPesa na Betin au kufanya hima kutafuta mdhamini mbadala.