• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
TEKNOHAMA: Simu haiathiri mtoto tumboni

TEKNOHAMA: Simu haiathiri mtoto tumboni

Na LEONARD ONYANGO

KILA mwanamke mjamzito hutarajia kujifungua mtoto mwenye afya njema asiye na dosari.

Ni kutokana na hili ambapo wataalamu wa afya wamekuwa wakiwashauri wajawazito kuepuka baadhi ya vyakula na hata pombe na mvinyo na vinywaji vingine ili kulinda afya ya mtoto aliye tumboni.

Kwa mfano, Shirika la Afya Duniani (WHO) linahimiza wanawake wanaopanga kupata mimba kujiepusha na pombe.

Mwanamke mjamzito anapokunywa pombe, mvinyo huo huingia moja kwa moja kwenye mishipa ya damu ya mtoto aliye tumboni.

Mtoto atazaliwa akiwa na matatizo mbalimbali kama vile kushindwa kuelewa chochote darasani, dosari katika ukuaji wa ubongo na mwili kukosa kukua vyema.

Wanawake wajawazito pia wanashauriwa kuepuka vyakula kama vile maziwa ambayo hajachemshwa, nyama ambayo haijaiva, mayai mabichi na vinywaji vyenye kafeini kama vile kahawa.

Mbali na vyakula, baadhi ya watu wamekuwa wakihofia kuwa wajawazito wanapotumia simu zao kwa muda mrefu huenda wanadhuru mtoto tumboni.

Hata hivyo watafiti wamejitokeza na kuondoa hofu hiyo kwa kusema kuwa matumizi ya simu hayaathiri kijusi tumboni.

Utafiti uliofanywa na wataalamu kutoka Taasisi ya Afya ya nchini Norway, ulionyesha kuwa mawimbi ya kielektroniki yanayotolewa na mtandao wa simu hayana athari kwa ukuaji wa ubongo wa mtoto aliye tumboni.

Dkt Eleni Papadopoulou aliyeongoza utafiti huo uliochapishwa katika jarida la BMC Public Health, alisema kwamba hawakupata ushahidi kwamba simu inasababisha watoto kushindwa kuzungumza vyema au kuelewa masomo darasani watakapokuwa wakubwa.

“Hatukupata ushahidi wowote wa kuhusisha matumizi ya simu miongoni mwa akina mama wajawazito na ukuaji duni wa ubongo wa watoto,” akasema.

Watafiti hao walihusisha akina mama wajawazito 45,389 na kuwagawa katika makundi mawili. Kundi la kwanza lilijumuisha wanawake wasiopenda kutumia simu mara kwa mara. Kundi jingine lilijumuisha waraibu wa simu.

Baada ya kujifungua, watafiti hao walifuatilia ukuaji wa ubongo wa watoto hadi umri wa miaka mitano.

Matokeo yalionyesha kuwa akili za watoto waliozaliwa na wanawake kutoka makundi yote mawili zilikuwa sawa.

“Utafiti wetu umebaini kwa mara ya kwanza kuwa utumiaji wa simu miongoni mwa akina mama wajawazito unaweza kuwa na manufaa badala ya madhara,” akasema Dkt Papadopoulou.

Kulingana na watafiti hao, watoto wa akina mama wanaotumia simu kwa wingi wakati wa ujauzito wana uwezo mkubwa wa kukumbuka, kusoma na kuzungumza kwa haraka ikilinganishwa na wenzao ambao mama zao hawapendi kutumia simu.

Wataalamu hata hivyo, wanaonya kuwa simu inaweza kuathiri tabia ya mtoto.

Hii ni kwa sababu wazazi hutumia muda mwingi kwenye simu badala ya kuzungumza na hata kucheza na watoto wao.

Mtoto kuathirika

Kwa mfano, mtoto anapotabasamu na asipate mtu wa kutabasamu naye huathirika katika ukuaji wa ubongo wake.

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa mtoto mchanga anahitaji kupapaswa mwili wake mara kwa mara.

Utafiti uliofanywa nchini Ujerumani na Singapore mwaka 2018 ulionyesha kuwa mtoto mchanga anahitaji kuguswa sawa na anavyohitaji chakula.

Kulingana na utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Cerebral Cortex, kumpapasa mtoto kunasaidia ukuaji wa mwili na akili.

Watafiti hao walikusanya watoto 40 wa umri usiozidi miaka mitano na kuwataka kucheza na mama zao kwa dakika 10 kwa muda wa siku kadhaa.

Baadaye, walibaini kwamba watoto waliokuwa wakiguswa na wazazi wao mara kwa mara wakati wa mchezo, walikuwa wachangamfu na wenye furaha na walitangamana na wenzao kwa urahisi.

Hivyo, wataalamu wanashauri wazazi kutenga muda mwingi wa kucheza na kutangamana na watoto wao badala ya kupoteza wakati mwingi wakitumia simu.

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Homa ya nyongo ya manjano katika watoto...

MAZINGIRA NA SAYANSI: Vipodozi vyarembesha ila pia hatari...

adminleo