• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
Umuhimu wa shukurani

Umuhimu wa shukurani

Na PHYLLIS MWACHILUMO

KWA hakika shukrani ni kitu cha maana sana licha ya kuwa huonekana kama jambo dogo tu.

Huweza kuelekezwa kwa Muumba kupitia sala au kwa binadamu wenzetu kwa kusema, “Asante!” kila mara unapotendewa jambo jema na mwenzako.

Bila shukurani, maisha hupungukiwa na ladha.

Bila shaka kunayo mambo chungu nzima ya kutufanya kutoa shukrani.

Baadhi ya hayo ni kama vile uhai, afya, mazingira mwanana na yenye starehe, kupata mahitaji ya kimsingi na kadhalika.

Wakati mwingine, mambo ‘madogo madogo’ yanapaswa kutushukurisha kama vile kuwa na wenzi ‘wanaotusumbua’ maishani kwani kunao watu wasiokuwa nao; pengine hata hali ya kuwa na hamu ya kula ila huna chakula ni jambo la kumtolea Maulana shukurani kwani kunao walio na kila aina ya malaji ila hamu ya kula hawana!

Maswala ya shukurani huendelezwa hata na viumbe kama vile majibwa wanaoonyesha kushukuru daima kwa riziki wapatazo kutokana na mabwana wao; seuze binadamu?

Kwa nini tuwe watu wa kulalama daima na kutotosheka? Lalama hizi ndizo huchangia maovu kila nui.

Vitabu Vitakatifu vinatuhimiza tuwe na mazoea ya kushukuru kwani mema yote yanatoka kwa Mwenye enzi. Mfano wa mafunzo haya yanapatikana katika Surah An-Nisa, Quran.

Ni vyema tutambue kuwa shukran ni chanzo cha mema mengi na furaha ya moyoni.

Iwapo tunajenga tabia ya kushukuru, basi huwa mwanzo wa unyenyekevu na hali ya kutosheka, hivyo basi, tunakuwa na furaha isiyo kipimo.

You can share this post!

TUZO KUU YANUKIA: Gwiji Cheruiyot, Kipchoge katika orodha...

Wapwani walalama kuchezewa na serikali

adminleo