USWAHILINI: Dera ni vazi linaloenziwa si Pwani tu, bali katika maeneo mengine pia
Na HAWA ALI
DERA ni aina ya vazi la kisasa la wanawake lililojiachilia.
Huvaliwa kwenye maeneo ya joto, hasa na Waswahili wa Pwani na huwa hariri la laini.
Ni vazi maarufu si kwa wanawake wa Pwani tu, bali pia wanawake wa maeneo ya bara humu nchini na hata kimataifa. Limekuwa maarufu kwa wanawake wa rika zote katika misiba mbalimbali, katika sherehe mbalimbali na kadhalika na wengine wanalipa heshima huku wengine wanalivunjia heshima.
Kulingana na baadhi ya watu dera ni nguo za nyumbani na mvaaji hafai kutoka nazo nje.
Dera ni vazi la heshima, lenye kusitiri mwili wa mwanamke vizuri sana, kama yalivyo kwa buibui na hijabu japo hayafuniki kichwa.
Kila mtu huvaa dera apendavyo. Wengine wanaweka kibwewe, wengine wanachanganya na nguo nyepesi ndani halafu inatokeza kidogo kwa chini, wengine huvaa na mkanda au mkufu ili kulibana katikati.
Yapo madera ya kila mtindo na gharama tofauti tofauti kulingana na uwezo wa mvaaji, lakini huvaliwa zaidi kwenye shughuli zenye stara kama vile msibani, kwenye dua mbalimbali kwa waislamu na hata vikao vya kanisani au jumuiya.
Dera linapendeza kila mtu. Halikatai mwili; ni wewe mwenyewe mvaaji kuchagua rangi inayokufaa na saizi yako.
Wanaodhani ni kuvaa dera ni uswahili ama ushamba, hawajui maana ya mavazi kwani hakuna vazi la mswahili wala mshamba, bali ni jinsi mvaaji atakavyopangilia mavazi yake na kuonekana nadhifu machoni pa watu.
Ukitembea Uswahilini, utakutana na wanawake wa huko wakiwa wamevaa dera kwani kwa miaka ya nyuma lilikuwa halijazoeleka, licha ya kwamba limekuwepo kwa miaka mingi kwenye ukanda wa pwani ambako buibui huwa ndilo vazi la kawaida.