Mashujaa Brigit, Eliud Kipchoge watua bila vifijo
Na GEOFFREY ANENE
WASHIKILIZI wa rekodi za dunia katika marathon, Brigid Kosgei na Eliud Kipchoge wamerejea nchini baada ya kupeperusha bendera ya Kenya vilivyo nchini Amerika na Austria, mtawalia.
Kosgei alishinda mbio za Chicago Marathon kwa saa 2:14:04, ambayo ni rekodi mpya ya dunia.
Alivunja rekodi ya saa 2:15:25 ambayo Muingereza Paula Radcliffe aliweka katika mbio za London Marathon mwaka 2003.
Pamoja na kocha wake Eric Maiyo, wameapa kuwa atavizia rekodi ya mbio za kilomita 21 ya dakika 64:51 inayoshikiliwa na Mkenya Joyciline Jepkosgei tangu mwaka 2017.
Pia, walifichua kuwa Kosgei ana mipango ya kuvunja rekodi yake ya dunia ya marathon kwa angaa dakika moja siku za usoni.
Akizungumza walipokaribishwa na Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) katika makao yake makuu kwenye jumba la Riadha House jijini Nairobi mnamo Jumatano asubuhi, Maiyo alisema kambi yake iko tayari kupimwa mara nyingi iwezekanavyo na Shirika la Kukabiliana na Matumizi ya Dawa ya kusisimua misuli nchini Kenya (ADAK) kuthibitishia ulimwengu kuwa alipata rekodi hiyo kwa njia halali.
“Brigid (Kosgei) hawezi kukwepa kupimwa. Tuko tayari kupimwa mara nyingi iwezekanavyo. Naapa kujiuzulu kazi ya ukocha ikiwa Brigid atapatikana na uovu wa kutumia njia ya mkato kupata ufanisi huo,” alisema kocha huyo.
Rais wa AK Jackson Tuwei pia alisisitiza umuhimu wa wanariadha kushindana bila kutumia dawa za kusisimua misuli akisema bado Kenya haijaondolewa katika orodha ya mataifa yanayomulikwa zaidi duniani kwa uovu huo.
“Baadaye mwaka huu, tutaandaa warsha na wanariadha wetu, hasa wale wanaoshiriki mbio za barabarani ili kuwapa mafunzo jinsi ya kuwekeza fedha zao, sheria mpya za Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) na vita dhidi ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli. Tutaalika pia makocha,” alisema Tuwei.
Katika hafla hiyo, ambayo pia Tuwei na viongozi wengine wa AK walimpongeza Kipchoge, Kosgei alihakikishia Wakenya kuwa yuko tayari kuiwakilisha nchi hii katika Michezo ya Olimpiki jijini Tokyo nchini Japan mwaka ujao.
Kipchoge alirejea kimyakimya kutoka Bara Ulaya alikotimka mbio maalum za INEOS 1:59 Challenge kwa saa 1:59:40 jijini Vienna, Austria na kuwa binadamu wa kwanza kukimbia mbio hizo za kilomita 42 chini ya saa mbili.