Makala

Kuridhia kwa neno 'asante' ni ishara unathamini wema uliotendewa

October 18th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

AGHALABU viongozi wengi wanapokamilisha kuzungumza au kutoa hotuba, neno asante au shukrani halikosi kuwatoka.

Kwa mfano, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya anapokunja jamvi hotuba, huhitimisha kwa kauli “Asanteni na Mungu awabariki na aibariki Kenya”. Aliyekuwa Rais wa Amerika Barrack Obama, alikuwa na mazoea ya kuhitimisha hotuba yake kwa maneno “asanteni, pia shukrani”.

Ni hulka inayoonyesha kuwa wameridhia hadhira kuwasilikiza na kuwapa maskio yao kwa hali na mali. Si eti hawana gange ya kufanya wakati huo, ila wana hamu ya kutaka kujua mzungumzaji ana yapi kueleza.

Ingawa, pia kuna wanaohudhuria mikutano ya hadhira kwa kuwa wanaozungumza ni watu mashuhuri au tajika.

Ufafanuzi wa kina, asante, ni neno tunalotumia mara kwa mara ambapo lengo lake ni kuwasilisha hisia njema kuhusu mambo tunayofanyiwa ama kupewa. Kimsingi, ni kuelezea kujali, kutambua thamani, heshima, shukrani na mengi ya kufanana na hayo.

Mzazi au mlezi kwa mtoto au watoto, anapokua humnoa kukumbatia neno hilo anapofanyiwa wema.

Ni malezi bora yanayoonesha kuweka nidhamu.

Methali; Wema hauozi na ukioza haunuki, inaambatana na kutendewa wema, ambapo ukipata msaada kutoka kwa anayekujua au asiyekujua na ulikuwa katika hali tete, utanakili katika shajara yako ya kumbukumbu.

Japo huenda ukakosa kumlipa kwa fedha aliyekutendea wema, utaishia kumsifu kwa ukarimu wake. Wema haulipiki, na machoni mwa Mwenyezi Mungu ni kuonesha utu na mapenzi kwa binadamu mwenza.

Hata hivyo, ni wangapi wanaothamini hisani waliyopokea kwa kujibu asante au shukrani?

Unapoonyesha hisia njema kwa ulichotendewa, inatoka moyoni au ni kushinikiza?

Ni suala pana ambalo wewe mwenyewe una jawabu lako. Kwa hakika ni busara kujenga mazoea kushukuru hata ikiwa msaada uliopokea ni kiduchu.

Kasisi Charles Kinyua wa Kanisa la Katoliki anachanganua mada hii kwa kueleza ikiwa kuna jambo linaloridhisha Mungu ni kuona unaridhia msaada uliopata, pasi kujali ni mkubwa au haba.

“Jamii ninayotoka tunasema mbuzi wa kupewa hakaguliwi meno, ukipokezwa ridhia na ushukuru kwa kusema asante. Hivyo basi, ni muhimu kukumbuka wema uliotendewa,” anasema Bw Kinyua.

Mtumishi huyu anasema si lazima uurejeshe kwa aliyekusaidia ukijaaliwa baadaye, ila unaweza kutendea mtu mwingine bila kujali dini, jinsia, tabaka, jamii au kabila analotoka.

Katika jukwaa hilo, Kasisi Kinyua anaeleza kwamba Mola ataendelea kujaalia aliyekuokoa na vilevile wewe mwenyewe.

Majanga kama vile baa la njaa, ajali, mafuriko na hata magonjwa, ni baadhi tu ya changamoto zinazozingira binadamu akiwa humu duniani.

Kulingana na Bw Kinyua wenye uwezo wanahimizwa kujitolea kwa hali na mali kuokoa waathiriwa.

“Nao, waathiriwa, washukuru kwa kuwa si wenye utu wa aina hiyo. Kadhalika, wanapaswa kujikakamua ili waondokee masaibu yanayowafika ili jamii iinuke,” anasema.

Martin Gitahi anakumbuka kana kwamba ilikuwa jana tu mwaka 2008 baada ya kukamilisha kozi inayohusiana na masuala ya utalii, alihangaika kwa muda wa miaka mitatu jijini Nairobi akitafuta ajira.

Juhudi zake ziligonga mwamba na hakuwa na budi ila kurejea nyumbani, Naivasha akiwa amevunjika moyo.

Hata hivyo, nyota ya jaha ilimfikia kupitia halati yake aliyemtafutia kazi ya kuuza nguo kuukuu, mtumba, ambapo alikutana na mtalii aliyemsaidia. “Shangazi alinitendea wema na kila mara sikusita kumshukuru. Ni kupitia dua nilikutana na mtalii aliyenisaidia kuenda Ujerumani nikajaliwa kupata kazi niliyosomea,” amafafanua Martin.

Kupitia mfano huo, Kasisi Charles Kinyua anahimiza tusikome kusaidia tunapoweza na wanaotukosea tujifunze kusamehe na kuwaombea mema. Akitilia mkazo wa kuthamini wema, anashauri haja ya watu kuheshimiana na kutakiana mema, akisema ndizo nguzo muhimu zaidi maishani zikiwa ni pamoja na kupendana kwa dhati.