• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
ANA KWA ANA: ‘Niko singo sana, bado namsaka Johnny…’

ANA KWA ANA: ‘Niko singo sana, bado namsaka Johnny…’

Na THOMAS MATIKO

JUMANNE wiki hii, diva wa Afro Pop, toto la Kinigeria Yemi Alade alitua nchini kwa ajili ya pati yake mahsusi aliyoiandaa katika ukumbi wa Blue Door katikati mwa jiji la Nairobi.

Hafla hii likuwa shughuli muhimu sana kwa Yemi ukizingatia kwamba alisafiri kwa masaa 18 kutoka Ulaya alikokuwa ili kuhakikisha anaifanikisha.

Haikuwa pati tu, bali ilikuwa sherehe mahususi ya kuitambulisha albamu yake ya nne Woman of Steel baada ya Kings of Queen (2004), Mama Africa (2016) na Black Magic (2017).

Kama kawa’, safu hii ilikuwa kwenye tukio na kufanikiwa kupiga stori na kichuna huyo.

Nafurahia kukutana nawe, umependeza kweli.

Alade: Nashukuru kakangu, nami nimefurahi kukutana nawe.

Hivi kweli huwa unapata muda wa kupumzika sababu muda wote ni kama upo pipani angani?

Alade: Duh! Yaani sijui nikuambieje. Kikweli kwangu kupumzika ni starehe kubwa ambayo mara nyingi nashindwa kuigharimia kutokana na kuwa na ratiba inayonibana sana. Ila mara moja moja nikipata fursa, mimi huchukua muda wa mapumziko kutuliza akili.

Kuna mtu ataona unaongopea, sababu kwa namna anavyoyaona maisha yako ni kama vile unaishi maisha ya anasa na raha tu.

Alade: Hahaha! Usinichekeshe. Ila wajua kila mtu ana uhuru wa mawazo yake. Lakini kwa mtu anayeelewa maisha ya msanii, basi atajua huwa nabanika sana. Kwa mfano kwa siku 12 zilizopita nimetalii mabara manne toka Ulaya, Asia, Marekani na sasa nimerudi nyumbani Afrika. Sio rahisi, asikudanganye mtu!

Albamu yako mpya ‘Woman of Steel’ ina tofauti gani na zilizopita?

Alade: Tofauti ni kubwa sababu naamini kwa kila albamu anayofanya msanii, inapaswa kuonyesha levo aliyofikia katika kipindi kile. Kwenye Woman Of Steel mimi ni mtu tofauti kabisa na yule wa miaka mitatu iliyopita. Najieleza zaidi, nimeimarika zaidi na kiwango changu cha usanii kimepanda.

Hizi pati umezifanya kwenye miji kadhaa; London, Paris, Lagos, na pia Amerika. Zina umuhimu gani?

Alade: Najaribu kujiweka karibu na mashabiki zangu. Hii safari napenda nikiwahusisha pia kwa ukaribu na ndio sababu nimechacharika kuhakikisha zimefanikiwa na zimenipa fursa ya kutangamana na baadhi yao ili pia kupata uelewa wa wanavyoipokea na wapi wanaamini naweza nikaboresha.

Baada ya Nairobi, pati nyingine ya namna hii itakuwa wapi?

Alade: Nairobi ndio mji wa mwisho wa pati ya uzinduzi wa Woman of Steel. Sasa narejea katika maisha yangu ya kawaida ya kupiga shoo na kurekodi muziki zaidi. Shoo ijayo nitakuwa Ethiopia kisha Marekani.

Mtindo unaoufanya sio wa kawaida na wasanii wenzako wa Nigeria, unaweza kufafanua zaidi?

Alade: Muziki wangu umejifuma zaidi katika utamaduni wa Afrika, yaani Afro Beats, ila una mchanganyiko wa Pop na RnB. Lakini licha ya mchanganyiko huo, huwa najitahidi kudumisha uhalisia wa Kiafrika.

‘Woman Of Steel’ ina wimbo uliotafasiriwa kwa Kiswahili ‘Poverty’, unajaribu kufanya nini hasa?

Alade: Jamani nimefanya makusudi kutokana na mapenzi makubwa ambayo nimekuwa nikipata kutoka Ukanda huu. Nimefanya kuwashukuru mashabiki wangu katika Ukanda huu. Ukiona nimeamua kujumulisha wimbo wa Kiswahili, basi amini nadhamini sana sapoti ninayopata kutoka Ukanda huu. Sichukulii kwa mzaha.

Hivi uliwahi kumpata Johnny?

Alade: Kaka bado nipo singo sana tu nala maisha.

Khuh! Uliamua kubania eti eeh?

Alade: Sio hivyo. Wajua kama kutongozwa natongozwa sana tena na wanaume wa kila haiba ila bwana bado sijabahatika kukutana na yule ambaye tunaendana. Isitoshe, kwa ratiba yangu hii, inakuwa vigumu kumpata ubavu mwelewa.

You can share this post!

KIKOLEZO: Filamu iligeuka nuksi kwao

Wiper yalambishwa sakafu huku ODM, Jubilee ziking’aa

adminleo