• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
CHOCHEO: Raha ya usingizi wa mahaba

CHOCHEO: Raha ya usingizi wa mahaba

Na BENSON MATHEKA

JE, unataka kuimarisha uwezo wako wa kutekeleza na kufurahia tendo la ndoa?

Basi, usijinyime usingizi wa kutosha.

Wataalamu wanasema kwamba watu wanaokosa kupata usingizi wa kutosha kila usiku, wanapunguza uwezo wao wa kutamba wakati wa shughuli chumbani. Wanasema kuwa kwa kawaida mtu anafaa kupata usingizi kwa saa saba kila usiku.

“Kujinyima usingizi wa kutosha kwa sababu moja au nyingine kunapunguza uwezo wako wa kutekeleza na kufurahia tendo la ndoa. Uhusiano wa usingizi na tendo la ndoa ni zaidi ya kuwa vitendo vyote hufanyika kitandani,” unasema utafiti uliochapishwa katika jarida la mtandaoni la Psychology Today.

Wanasaikolojia wanasema watu wanaopata usingizi wa kutosha huwa mabingwa wa kula uroda na wanaopenda kula uroda huwa wanapata usingizi wa kutosha. “Ikiwa hupati usingizi wa kutosha, nguvu za kurindima chumbani huwa zinapungua. Kwa upande wa wanawake, hukosa raha ya kuchangamkia na kufurahia tendo la ndoa,” unaeleza utafiti huo.

Wataalamu wanasema mtu anaweza kuimarisha uwezo wake wa kula uroda kwa kuhakikisha anapata usingizi wa kutosha.

Utafiti huo unasema kwamba kukosa usingizi wa kutosha kunasababisha mfadhaiko na matatizo ya ubongo, hali za kiafya ambazo hufanya mtu kupungukiwa na uwezo wa kupandisha mzuka chumbani. “Katika hali hii, ubongo hukosa kutoa homoni za estrogen na testosterone zinazoimarisha uwezo wa wanawake na wanaume kutekeleza tendo la ndoa,” wanaeleza watafiti.

Wanaeleza kuwa kwa wanawake hali hii hutokana na mimba, kukoma kupata hedhi na mtindo wa maisha. “Mwanamke akipata mtoto, huwa anatatizika kupata usingizi akimshughulikia na hii huwa inaathiri uwezo na hamu yake ya tendo la ndoa,” wanaeleza wataalamu.

“Kukosa usingizi wa kutosha huwa kunafanya uhisi uchovu na imebainika kupitia tafiti nyingi kuwa watu wengi huwa hawawezi kushiriki au kufurahia chumbani wakiwa wachovu,” asema mwanasaikolojia Dennis Gathuku wa shirika la Big Hearts, jijini Nairobi.

Kulingana na utafiti uliofanywa na chuo kikuu cha Michigan, Amerika, watu wanaopata usingizi kwa masaa mengi huwa wanachangamkia uroda zaidi siku inayofuata.

Bw Gathuku anasema tafiti zimeonyesha kuwa kufanya mapenzi kabla ya kulala, hukufanya kupata usingizi mwanana. Hii ni kwa sababu hufanya mwili kutoa homoni za endorphins zinazosaidia katika usingizi.

Wataalamu wa usingizi wanasema kuwa unafaa kujiepusha na hulka zinazoweza kukunyima usingizi wa kutosha kama vile matumizi ya bidhaa zenye kafeni.

Kulingana na mwanasaikolojia Dkt Thaddeus Wekesa, unapaswa kufanya mazoezi kwa dakika zisizopungua 30 kila siku ili kuimarisha usingizi.

Aidha unashauriwa kuhakikisha chumba cha kulala kina hewa safi ya kutosha na hakina mwangaza unaoweza kuwatatiza. Wanapendekeza kuzima simu za mkono, redio na runinga katika vyumba vya kulala ili kupata usingizi mwanana.

Ingawa wataalamu wanasema kufanya mapenzi sio njia ya pekee ya kupata usingizi mzuri, wanakubaliana kuwa usingizi tosha bila shaka unaimarisha uwezo wa mtu kuwika chumbani.

“Usingizi wa kutosha unakuhakikisha stamina na nguvu za kutekeleza tendo la ndoa. Usingizi pia hufanya mwili kudhibiti homoni na kukuandaa tayari kwa tendo la ndoa,” unaeleza utafiti wa Psychology Today.

Wanasema kwa jumla usingizi ni muhimu kwa afya ya mtu.

You can share this post!

FUNGUKA: ‘Nimemweka mahali pema moyoni…’

DAU LA MAISHA: Ugonjwa haujazima moyo wa ukarimu

adminleo