Ghasia zapangua gozi la El Clásico
Na MASHIRIKA
MADRID, Uhispania
GOZI maarufu la El Clásico kati ya mahasimu wa tangu jadi Barcelona na Real Madrid, ambalo liliratibiwa kusakatwa Oktoba 26 uwanjani Camp Nou, limepanguliwa kutokana na ghasia katika eneo la Catalonia.
Likitangaza Ijumaa hatua ya kuahirisha mchuano huo, Shirikisho la Soka nchini Uhispania (RFEF) lilipatia klabu hizi mbili makataa ya Jumatatu saa tano asubuhi kuafikiana tarehe mpya.
RFEF imesema itafanya uamuzi ikiwa miamba hawa wawili hawataafikiana kuhusu tarehe mpya.
“FC Barcelona na Real Madrid lazima zikubaliane tarehe mpya ya kukutana kabla ya Oktoba 21,” taarifa ya RFEF ilisema.
“Zisipofikia mapatano, basi Kamati ya Mashindano itawajibika kutangaza tarehe mpya.”
Tarehe mbili za siku mpya ya mechi zilizowekwa mezani ni Jumatano ya Desemba 18, wakati timu zingine za Uhispania zitajitosa katika dimba la Copa del Rey, na Jumamosi ya Desemba 7.
Mechi hii ya Clasico iliratibiwa kuwa ya kwanza ya nyumbani ya Barcelona tangu viongozi tisa wanaotaka eneo la Catalonia kuwa taifa tofauti na Uhispania wasukumwe jela kwa kati ya miaka tisa na 13 hapo Jumatatu kwa kuandaa kura ya maoni ya eneo hilo kujitenga ambayo haikuwa ya halali mwaka 2017.
Hukumu ya kufungwa jela ilizua rabsha kote mjini Barcelona na kulikuwa na wasiwasi kuwa waandamanaji watatumia Clasico kufanya maandamano zaidi.
Klabu ya Barcelona, ambayo inachukuliwa na wakazi wa Catalonia kama ishara ya eneo hilo, ilijibu katika taarifa Jumatatu ikisema kuwa “adhabu ya kuwekwa jela si suluhisho”.
Uwanja
La Liga kisha ikapendekeza kwa RFEF kuwa uwanja wa mchuano huo wa Clasico ubadilishwe kutoka Camp Nou hadi ule wa Madrid wa Santiago Bernabeu, ingawa klabu hizi hazikuwa tayari kukubali mabadiliko hayo.
“RFEF imefutilia mbali ombi la La Liga kuhusu kubadilisha uwanja wa mechi kati ya Barcelona na Real Madrid,” taarifa iliongeza. Badala yake, iliamuliwa kuwa tarehe ndio itabadilishwa kwa kile RFEF ilitaja kuwa “hali isiyo ya kawaida”.
Baada ya kura ya maoni ya Catalonia ya mwaka 2017 ya eneo hilo kutaka kujitawala, Barcelona ilisakata mechi moja ya ligi dhidi ya Las Palmas bila mashabiki kulalamika ombi lao la kutaka iahirishwe kukataliwa.
Barca itazuru Eibar leo na ilitarajiwa kusafiri kilomita 589 kwa kutumia basi ili kuepuka maandamano katika uwanja wa ndege wa El Prat. Real Madrid pia iko ugenini leo dhidi ya Real Mallorca.