Makala

MUTUA: Ni kweli Uhuru hatatumia BBI kujitengenezea cheo?

October 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na DOUGLAS MUTUA

WAUTEMAO Umombo kwa ufasaha watakwambia kuwa uvumi husalia uvumi hadi utakapokanushwa.

Kimsingi, hilo likanushwalo ndilo, usidanganyike eti.

Katika muktadha wa siasa za Kenya, haswa mabadiliko ya kikatiba yanayopendekezwa na mrengo mmoja wa serikali na mwingine wa upinzani, huenda usemi huu una ukweli.

Rais Uhuru Kenyatta amesimama kidete juzi kukanusha uvumi kwamba juhudi za kuigeuza Katiba, almaarufu kama BBI, ni njama yake kusalia madarakani baada ya 2022.

Wajuaji kwenye vichochoro vya kisiasa wanadai mpango huo unanuiwa kuwapa wanasiasa wakuu fursa zaidi za kushikilia madaraka hata wakibwagwa kwenye uchaguzi.

Mpango wenyewe ni zao la ule mkono wa maridhiano kati ya marafiki wapya, Bw Kenyatta na kinara wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Bw Raila Odinga.

Unashukiwa na wasiowaunga mkono wawili hao kwamba unanuiwa kubuni vyeo vya waziri mkuu, manaibu wake wawili, manaibu wawili wa rais na kadhalika.

Fununu zinaeleza kwamba, kwa kuwa Bw Kenyatta atamaliza kipindi chake cha pili ifikapo 2022, atahamia kwenye wadhifa wa Waziri Mkuu naye Raila awe Rais.

Ni madai hayo ambayo yametokea kumkasirisha Bw Kenyatta mno kiasi cha kuyakanusha kila anapopata fursa ya kufanya hivyo.

Wanaoshuku kwamba mpango huo wa kugawana madaraka upo wanashikilia kwamba ni njama ya kisiasa dhidi ya Naibu Rais, William Ruto, anayeaminika kutopatana na Bw Kenyatta.

Si vigumu kuelewa madhumuni ya Bw Odinga katika njama kama hiyo kwa maana ni dhahiri safari yake ya kuingia Ikulu, hata kwa siku moja tu, haijavunjika.

Lakini, ikiwa kweli njama dhidi ya Bw Ruto ipo, chanzo chake ni kitendawili ambacho kinaweza tu kuteguliwa naye mwenyewe pamoja na huyo mkubwa wake.

Dalili zote zinaonyesha kwamba kwa hakika uhasama kati ya Rais na Naibu wake upo, hasa ikizingatiwa kwamba Rais ananufaika na uungwaji mkono na upinzani bungeni huku Bw Ruto akionekana kushupaza shingo.

Binafsi sishangazwi na tendo la Bw Kenyatta kughairi nia ya kumuunga mkono Bw Ruto kuurithi urais kama alivyoahidi kadamnasi ya watu mnamo 2013.

Ahadi za kisiasa huaminiwa na mjinga pekee. Anayezitimiza pia huwa kakosa manufaa ya kuzivunja, hali ambayo sidhani Bw Kenyatta amejipata akipambana nayo.

Wanaomhimiza awe Waziri Mkuu wanasema angali ‘mchanga’, hajatimu umri wa kustaafu, hivyo maarifa yake ya kiutawala yasiruhusiwe kuozea nyumbani akistaafu.

Tofauti

Hatujui Bw Kenyatta ameona kitu gani kumhusu Bw Ruto asichoridhia, akasalitika kumuunga mkono Raila, aliyekuwa hasidi wao mkuu katika chaguzi za 2013 na 2017.

Hata hivyo si ajabu. Unaposoma makala haya, kiongozi wa muda mrefu wa Botswana, Jenerali Ian Khama, ambaye alistaafu mwaka jana, anafanya kampeni dhidi ya aliyekuwa naibu wake.

Jenerali Khama mwenyewe alimteua Rais wa sasa, Bw Mokgweetsi Masisi, kumrithi akiamini kwamba angekuwa kiongozi bora. Lakini uchu wa kudhibiti chama tawala ulizua uhasama kati yao.

Sasa Jenerali Khama anazunguka nchi nzima akiwaambia watu wamchague Bw Duma Boko, hasidi wake wa tangu jadi, katika uchaguzi utakaofanyika Jumatano hii.

Je, huenda tukashuhudia hali kama hiyo nchini Kenya wakati wa kampeni za 2022, yaani Bw Kenyatta akimpigia debe Bw Odinga dhidi ya Naibu wake mwenyewe, Bw Ruto?

Kabla ya kujua iwapo hilo linawezekana, kwanza tukumbuke mabadiliko ya Katiba yanayopendekezwa ni sharti yawekwe kwenye mizani na wananchi kupitia kura ya maamuzi.

Ni baada ya shughuli hiyo ambapo miungano mipya ya kisiasa itaibuka, wanasiasa wengi wa ngazi ya chini wajiunge na upande utakaoshinda.

Iwapo Bw Ruto atafanikiwa kuwashawishi wananchi kuyakataa mabadiliko hayo, basi nakutabiria Bw Kenyatta na Bw Odinga wajiandae kustaafu kutoka katika siasa.

Na ikitokea kwamba Bw Ruto atashindwa katika kura ya maamuzi, basi itabidi aanze kufanya mazoezi ya kuikabili serikali kama kiongozi wa upinzani kuanzia 2022. Langu nawe ni jicho tu hadi hapo.

[email protected]