Habari

Afisa wa polisi ajitoa uhai mjini Ruiru

October 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na LAWRENCE ONGARO

AFISA mmoja wa polisi katika kituo cha Ruiru alijitoa uhai Ijumaa usiku katika chumba chake.

Afisa mkuu wa polisi wa Ruiru Bw Phineus Ringera, amethibitisha kifo hicho huku akisema kiini hasa cha kujitoa uhai kwa mwendazake hakijaeleweka vyema.

Afisa huyo alipohojiwa zaidi amesema hakuwa tayari kusema lolote kuhusu kitendo hicho kwa vile bado walikuwa wakitaka kujua hasa kilichojiri ili waweze kuwa na picha kamili ya jambo hilo.

“Kwa wakati huu sitaki kusema lolote kuhusu kifo chake, kwanzaac ha tufanye uchunguzi ili tuweze kuongea zaidi. Pia ni lazima tuifahamishe familia ya marehemu,” alisema Bw Ringera.

Kituo cha Polisi cha Ruiru kilifurika watu waliotaka kujua hasa chanzo cha kujitoa uhai kwa afisa huyo wa polisi.

Inadaiwa ya kwamba maafisa wenzake waliokwenda kwake majira ya asubuhi walipata chumba chake kimefungwa kwa ndani. Lakini baadaye walipoingia walipata amejinyonga mle ndani.

Kila mmoja aliyekuwa katika eneo hilo alionyesha hali ya mshangao huku wakijadiliana kwa sauti za chini.

Hakuna yeyote aliyetaka kueleza alilojua kuhusu kisa hicho kwani wengi wao hawakuwa na ufahamu ni jambo lipi lililofanya afisa huyo kujitoa uhai.

Hata hivyo uchunguzi uliofanywa umebainisha ya kwamba maafisa wengi wanapitia masaibu mengi ya kisaikolojia; hasa maswala ya kikazi na ya kifamilia.

Yote hayo yakitathminiwa kwa makini yanachangia masaibu kadha yanayowakumba maafisa wengine kikosini.

Wakati huo huo pia, kuna maswala ya kufanya kazi muda mrefu bila kupata muda ufaao wa kupumzika.

Iliripotiwa kuwa miezi miwili iliyopita, afisa mwingine wa polisi alijitoa uhai katika kituo hicho cha Ruiru, jambo ambalo linazua maswali mengi kuhusu maafisa hao kujitoa uhai.