• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
Kenya Sevens sasa yatupia macho mchujo wa Olimpiki

Kenya Sevens sasa yatupia macho mchujo wa Olimpiki

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Kenya inaangazia sasa Kombe la Afrika mnamo Novemba baada ya kurejesha taji la shindano la Tusker Safari Sevens mnamo wikendi jijini Nairobi.

Vijana wa kocha Paul Feeney, ambao walimaliza makala ya 23 ya Safari Sevens katika nafasi ya kwanza (Morans) na tatu (Shujaa), wamechukua mapumziko mafupi halafu warejelee mazoezi ya Kombe la Afrika litakalofanyika Novemba 8-9 uwanjani Bosman mjini Johannesburg.

Kenya ni mabingwa wa Afrika mwaka 2004, 2008, 2013 na 2015.

Walipata mataji yao matatu ya mwisho kwa kupiga Zimbabwe 26-14, 24-19 na 19-17, mtawalia.

Makala ya mwaka 2015 pia yalitumiwa kuchagua mwakilishi wa Bara Afrika kwenye michezo ya Olimpiki mwaka 2016. Kenya ilinyamazisha Zimbabwe 19-17 katika fainali ya mwaka 2015 na kufuzu kushiriki makala ya kwanza ya raga ya wachezaji saba kila upande kwenye Olimpiki jijini Rio de Janeiro, Brazil.

Mashindano ya mwaka huu pia yatashuhudia bingwa wa Afrika akijikatia tiketi ya kushiriki Olimpiki jijini Tokyo nchini Japan mwaka 2020.

Mabingwa wa mwaka 2000, 2012 na 2018 Zimbabwe na wafalme wa mwaka 2016 na 2017 Uganda pamoja na Ivory Coast, Madagascar, Zambia, Tunisia, Senegal, Morocco, Namibia, Ghana, Botswana, Mauritius na Nigeria, wanakamilisha orodha ya timu zinazotarajiwa kukusanyika mjini Johannesburg kuwania taji la Afrika na tiketi ya kushiriki Olimpiki. Zimbabwe ilinyakua taji la mwaka jana kwa kuzaba Kenya 17-5 mjini Monastir nchini Tunisia.

Mshindi wa Afrika mwaka 2019 ataungana na wenyeji Japan kwenye Olimpiki.

Mataifa mengine yaliyofuzu kushiriki Olimpiki ni Fiji, Amerika, New Zealand na Afrika Kusini yaliyokamilisha Raga ya Dunia ya msimu 2018-2019 katika nafasi nne za kwanza na mabingwa Argentina (Amerika Kusini), Canada (Amerika Kaskazini) na Uingereza (Bara Ulaya). Kanda za Oceania na Bara Asia zitachagua wawakilishi wao Novemba.

Timu zitakazokamilisha mashindano ya Afrika katika nafasi ya pili na tatu zitafuzu kupigania tiketi moja kutoka kwa mchujo wa dunia wa Olimpiki mwezi Juni 2020 dhidi ya Brazil, Chile, Jamaica, Mexico, Ufaransa, Ireland na nambari mbili na tatu kutoka Oceania na Asia.

Kwingineko, Kenya italimana na wakali Afrika Kusini na Uingereza pamoja na Uhispania kwenye mechi za Kundi D za duru ya ufunguzi ya Raga ya Dunia ya msimu 2018-2019 itakayoanza mnamo Desemba 5.

Shujaa itapepetana na Afrika Kusini mnamo Desemba 5 na Uingereza na Uhispania mnamo Desemba 6.

Kundi A linaleta pamoja Fiji, Ufaransa, Argentina na Japan nazo Marekani, Australia, Scotland na Ireland zinapatikana katika Kundi B. New Zealand, Samoa, Canada na Wales ziko katika Kundi C.

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Upasuaji wa titi ulivyomzidishia karaha...

MSWAKI: Vikosi vya Uingereza kuwa na mteremko

adminleo