Makala

'Kadhia za mafuriko zinaweza kuepukika serikali ikijipanga'

October 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

MZAWA wa Kaunti ya Murang’a Njeri Ndiritu anakumbuka jinsi ambavyo rafiki yake wa dhati aliangamia pamoja na mume wake na watoto wake kupitia maporomoko ya ardhi.

Anakumbuka kama jana.

Murang’a inafahamika kwa milima na mabonde, na walikuwa wakiishi eneo la aina hiyo.

Miaka kadhaa iliyopita, familia hiyo ilikumbana na mauti maji ya mvua yaliposomba udongo na miti na makazi yakafunikwa.

“Tulipoamka tulianza kuulizana nyumba yao ilikoenda, waliokuwemo walikuwa ‘wamezikwa’ humo,” anaeleza Bi Njeri.

Ni mtoto mmoja pekee wa familia hiyo aliyesalia, na aliponea tundu la sindano kwa kuwa alikuwa ameenda kutembelea shangazi yake.

Taswira hiyo ni sawa na inayoshuhudia sasa maeneo mbalimbali nchini kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha.

Kulingana na idara ya utabiri wa hali ya hewa inaonya kuwa mvua hiyo huenda ikaendelea hadi Februari 2020.

Mwezi Oktoba hadi Desemba, Kenya hupokea mvua ya kipindi kifupi.

“Kuna uwezekano kupokea mvua kubwa kuliko ya msimu mrefu, hasa maeneo yanayopata ile haba. Huu ndio msimu utaskia miti ikiangukia nyumba na mapaa kupeperushwa,” anatahadharisha Ezekiel Muigai wa kutoka kitengo cha kitaifa cha utabiri wa hewa nchini.

Kwa mujibu wa idara hiyo, zaidi ya kaunti 20 zinatajwa kuendelea kupokea mvua kupita kiasi.

Zinajumuisha Isiolo, Embu, Garissa, Kitui, Mombasa, Nyeri, Makueni, Homa Bay, Turkana, Meru, Kiambu na Kwale, miongoni mwa nyinginezo.

Tayari athari zake zimeanza kushuhudiwa ambapo watu kadhaa wameripotiwa kufa maji Kitui, Meru, na Garissa.

Katika kaunti ya Elgeyo Marakwet, familia ya watu wanne iliripotiwa kuangamia wiki iliyopita, kufuatia maporomoko ya ardhi na udongo uliofunika nyumba yao.

Mbali na makazi, baadhi ya maeneo barabara hazipitiki kwa ajili ya mafuriko. Ni hali tete inayotishia kusababisha mkurupuko wa maradhi kama vile Kipindupindu.

Serikali za kaunti zilizotajwa kuathirika pamoja na asasi husika, wanahimiza watu kuondoka maeneo hatari, hasa wanaoishi karibu na kingo za mito, bahari na milima na mabonde.

“Iwapo barabara imefurika, wendeshaji magari msijaribu kuitumia. Ninahimiza Wakenya waepuke maeneo hatari,” anashauri Samuel Mwangi, naibu mkurugenzi idara ya hali ya anga nchini.

Kenya, kuna kitengo cha kitaifa kinachokabiliana na kuangazia majanga ya dharura (NDMU.

Kinapaswa kuwa ange na kufanya kazi kwa karibu na idara ya utabiri wa hewa, ambapo kinafaa kuwa kikitoa taarifa kila wakati kuhusu majanga ibuka.

“Kinapojua hali ilivyo, kifanye hamasisho ili kutahadharisha wananchi, kwa kushirikisha wadau wote,” apendekeza Njeri Ndiritu. Hapa nchini, imekuwa mazoea serikali kuchukua hatua majanga au maafa yanapotokea.

Kenya ni taifa lenye ukwasi usiomithilika, na serikali inapaswa kutilia mkazo majanga kwa kutenga fedha za dharura kuyakabili. Mataifa yaliyoimarika kimaendeleo, huwa yamejiandaa kwa chochote ambapo ni nadra kuskia maafa.

Kwa sasa mvua kubwa na mafuriko yanatikisa vichwa vya vyombo habari, na miezi kadhaa baadaye habari kuu zitakuwa njaa.

Ni suala linaloibua maswali chungu nzima kuhusu utendakazi wa serikali.

Taifa kama Israili mvua inayonyea, linahakikisha hakuna hata tone moja linalopotea. Uvunaji wa maji Israili umepewa kipau mbele, ambapo msimu wa mvua hutekwa kwa mabwawa na vihifadhio.

Aidha, huyatumia kufanya shughuli za kilimo. Israili ni tajika katika uzalishaji wa nafaka na matunda. Ni hatua ambayo ikiigwa na serikali ya Kenya, suala la maji kupotea na maafa yanayosababishwa na mafuriko litakuwa historia.

Mkondo wa maji ukitengenezwa, na kuelekezwa kwenye mabwawa, si hatari ya mafuriko pekee itakayoondolewa ila maji yatatekwa na kuvunwa, yatumike msimu wa kiangazi kufanya kilimo.