SEKTA YA ELIMU: Mageuzi yanahitajika katika elimu ya vyuo vikuu ili ikidhi mahitaji ya kiajira
Na CHARLES WASONGA
VYUO vikuu vya humu nchini vimelaumiwa kwa kuzalisha wahitimu wasio na ujuzi hitajika katika soko la ajira nchini.
Hii inachangiwa na hali kwamba baadhi ya kozi zinazofundishwa katika vyuo hivyo hazijaambatanishwa masuala yanayopewa kipaumbele katika ajenda za maendeleo nchini, mathalani, sayansi na fani mbalimbali za teknolojia.
Hali ya sasa ambapo vyuo hivyo havina uwezo wa kutoa elimu tekelezi imehusishwa na uwepo wa idadi kubwa ya wahitimu kukosa ajira na/au uwezo wa kujiajiri wenyewe.
Takwimu kutoka Shirika Kitaifa la Takwimu (KNBS) na zile za Benki ya Dunia (WB) zinaonyesha kuwa, kwa wastani, vijana 800,000 hujiunga na soko la ajira kila mwaka baada ya kuhitimu kutoka vyuo vikuu na vile vya kadri.
Waajiri wanalalama kuwa wao hulazimika kutumia rasilimali nyingi kuwapa mafunzo zaidi wahitimu hawa ili waweze kumudu kazi walizoajiriwa kwayo.
Na ili kubadili kukabiliana na udhaifu huo vyuo vikuu vya umma nchini sasa vimeandaa mikakati ambayo kwayo vinalenga kuwafinyanga wanafunzi ambao, baada ya kuhitimu, watakuwa wabunifu katika taaluma walizosomea.
Mojawapo ya mikakati hiyo ni mageuzi ya mitaala inayofundishwa katika vyuo hivyo.
Kamati ya Manaibu Chansela wa Vyuo Vikuu vya Umma, katika ripoti yake iliyotolewa Julai mwaka huu, inapendekeza kuwa mabadiliko katika mitaala inayofundishwa katika vyuo hivi ili ioane na mahitaji malengo ya maendeleo nchini.
Kamati hii inasema vyuo vikuu vinapasa kufundisha kozi zilizoidhinishwa na Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu (CUE) pekee, ili kuzuia dhana kwamba baadhi ya kozi zinazofunzwa katika vyuo vikuu sio halali.
“Huu mtindo wa baadhi ya vyuo kuanzisha kozi kiholela bila kutafuta idhini kutoka CUE unafaa kukoma. Na kozi zenyewe zapasa kuoanishwa na ajenda za maendeleo ya serikali. Kozi zinazowezesha vyuo vyetu kuzalisha wataalamu wabunifu,” ripoti hiyo inasema.
Itakumbukwa kuwa mnamo Februari 2019 tume hiyo ilifichua kuwa jumla ya kozi 133 zinazofunzwa katika vyuo vikuu vya umma na vya kibinafsi ni batili kwani zilianzishwa bila idhini yake, kulingana na sheria. Vilevile, tume hiyo ilisema baadhi ya vyuo zimekuwa zikianzisha kozi fulani ilhali havina wahadhiri na vifaa hitajika kuzifundisha.
Ripoti hiyo ya kamati ya magavana pia inapendekeza kwamba vyuo vikuu vianzishwe kwa misingi ya uwezo wavyo katika ufundishaji wa kozi au taaluma.
Hatua hiyo inalenga kurejeshwa katika hali ilivyokuwa zamani ambapo kila chuo kikuu kilijikita katika ufundishaji wa taaluma fulani.
Kwa mfano, Chuo Kikuu cha Kenyatta kilikuwa mahiri katika mafunzo ya taalama ya ualimu, chuo kikuu cha Nairobi kikifahamika kwa taaluma kama vile uanasheria, udaktari na utawala.
Na chuo kikuu cha Egerton kilibobea katika ufundishaji wa kozi za kilimo nacho chuo cha kilimo na teknolojia kikifahamika kama kitovu cha kufundishia kosi za teknolojia na utafiti wa kisayansi.
“Mwelekeo kama huu utawezesha vyuo vikuu kutafuta ufadhili kutoka humu nchini na ng’ambo kwa ajili ya kuendelea taaluma mahsusi zinazofundisha kando na kufanya tafiti zaidi katika nyanja husika. Kwa namna hii vyuo vitaweza kuzalisha wahitimu wenye ujuzi hitajika kujiajiri au kupata ajira,” ripoti hiyo ya manaibu chansela inasema.