Habari

Bima ya Afya: Jubilee iliwahadaa wakongwe mwaka 2017?

October 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

JUMLA ya wazee 484 kote nchini ambao walifaa kupata huduma za afya bila malipo chini ya mpango wa serikali wa Inua Jamii hawajakuwa wakipata hudumu hizo kwa sababu serikali haijatoa fedha ilizoahidi mwaka 2017.

Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa Hazina ya Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF) Nicodemus Odongo aliwaambia wabunge Jumatano kwamba licha ya wazee hao kupewa kadi za hazina hiyo, hawawezi kupata huduma ya afya kwa sababu serikali haijatoa Sh2.2 bilioni kufadhili mpango huo.

“Kadi za NHIF ambazo wazee hao walipewa mnamo 2017, haziwasaidii kupata matibabu katika hospitali zilizoweka mkataba nasi kwa sababu hazina ya kitaifa haijatoa pesa. Tukipokea Sh2.2 bilioni ambazo serikali iliahidi kadi hizo zitafanyakazi mara moja,” akawaambia wabunge hao ambao ni wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Afya.

Wanachama wa kamati hiyo; Swarup Mishra (Kesses), Eseli Simiyu (Tongaren) na David Ochieng’ (Ugenya) walikuwa wametaka kujua ni kwa nini wazee waliosajiliwa kwa mpango huo hawajakuwa wakipata huduma za afya bila malipo.

Hii ni licha ya serikali ya Jubilee kuzindua mpango huo maarufu kama ‘Inua Jamii 70 Plus’ miezi miwili kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.

“Tumepata ripoti kutoka kote nchini kwamba wazee wamekuwa wakiteseka kwa kukosa huduma za afya licha ya kuwa na kadi za NHIF walizopewa miaka miwili iliyopita. Mbona hawapati huduma ilhali serikali iliahidi kuzigharimia?” akauliza Dkt Mishra ambaye ni naibu mwenyekiti wa kamati hiyo

Septemba 2019 kundi la wazee katika kaunti ndogo ya Kajiado Kaskazini lilifika katika ofisi za afisa anayesimamia mpango wa Inua Jamii eneo hilo wakitaka kurejesha kadi za NHIF kwa msingi kuwa haziwasaidii

Afisa huyo Bw Daniel Nkoonka aliwafahamisha kwamba ofisi yake haiwezi kuwasaidia kwa njia yoyote “kwa sababu serikali haijatuma fedha za kufadhili mpango huu ili kadi zenu zifanye kazi.”