• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:55 AM
KIU YA UFANISI: Aliona washonaji nguo ni wengi, akaamua heri awe fundi wa pazia

KIU YA UFANISI: Aliona washonaji nguo ni wengi, akaamua heri awe fundi wa pazia

Na STEPHEN ODANGA

BI Mary Colleta Atieno ni fundi stadi wa kushona vitambaa na mapazia makubwa maridadi ya kuweka ukutani, kwa madirisha na pia kwa milango mikubwa hasa ya vyuo na ofisi.

Ukimwona mama Mary unaweza kudhani ni wa janibu za kutoka maeneo ya Nakuru au maeneo yanayopakana na Mlima Kenya lakini la. Mama Chris anasema yeye ni mzaliwa wa sehemu inayoitwa Jera, eneobunge la Ugenya, Kaunti ya Siaya.

‘Mama Chris’ kama anavyofahamika zaidi anafichua kwamba anapenda kazi yake kwa sababu haina ushindani kama kushona nguo.

Anaongeza kwamba mafundi wa nguo ni wengi zaidi na wametapakaa kila mahali, ndiposa akaamua kujitosa kwa ufundi wa kushona pazia.

‘Mama Chris’ anaendelea kufichua kwamba alijifunza kushona pazia mwaka wa 2002 katika chuo kinachojulikana kama Amedo Dressmaking and Embroidery, Nakuru.

Ushindani

Mwaka wa 2004 – ikiwa ni miaka miwili baada ya kuhitimu – ‘Mama Chris’ alianza kufanya kazi yake mjini Nakuru ambako anasema palikuwa na ushindani wakati huo.

Alifanya kazi kwa miaka minne na mwaka wa 2008 alisafiri na kuja kufanya kazi katika mji wa Bumala kaunti ya Busia. Bumala ni mji mkubwa na wakati akija palikuwa hakuna fundi wa kushona pazia hata mmoja jambo lililompa umaarufu zaidi.

Pazia moja huuzwa kwa kati ya Sh4,500 na Sh6,000 na pia yategemea na ukubwa, aina ya kitambaa na pia muundo wa pazia. Kando na kushona pazia anauza pia curtain rods, curtain tapes, curtain rings na vifaa vingine vya kuunda pazia na vitambaa. Ama kweli wahenga walisema “Bahati ni bidii” kwa sababu huwezi kubahatika na kufanikiwa kama huna bidii.

Kazi ilinoga na mwaka wa 2016 akapata kandarasi ya kushona pazia kwa chuo kikuu cha Benga, eneobunge la Butula, kaunti ya Busia.

Kazi hii ilimpa pesa nyingi na Mwaka wa 2017, kazi yake ilikuwa imevutia wateja wengine kama vile ofisi za C.D.F eneo hilo la Butula walimtafuta na kumpa kazi kubwa ya kuunda pazia kwa majengo yote ya ofisi zao.

Kwa ajli ya kupata kazi nyingi kwa karakana yake ilimbidi aajiri msaidizi aliyehitimu kushona pazia, Rose Pamela ambaye wanafanya naye kazi hadi leo. Kando na kushona pazia katika karakana yake, mama Chris pia hutoa mafunzo kwa wale wanaotaka kujifunza kushona pazia.

Anasema mafunzo huchukua kati ya miezi sita na mwaka mmoja na nusu na malipo huwa ni Sh1,500 kwa mwezi. Kufikia wakati wa kuandika makala haya, mama Chris alikuwa na mwanafunzi mmoja, Quinter Aluoch, ambaye sasa amebakia muda mfupi tu aweze kuhitimu ushonaji wa pazia na vitambaa.

Mama Chris anasema yuko tayari kusaidia fundi yeyote ambaye anataka kujua kushona pazia kutoka kaunti hii ya Busia au kaunti ya Siaya.

Unaweza kuwasiliana naye kupitia nambari za smu 0723 944 299 kwa maelezo zaidi kuhusu jinsi wataka kusaidiwa au kama wataka kushonewa pazia.

You can share this post!

KILIMO NA UCHUMI: Mateso aliyopata mjini yalimfanya arejee...

CITY NOMA: Manchester City yaipiga Atalanta 5-1

adminleo