• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:03 PM
BONGO LA BIASHARA: Sehemu yake ya biashara ya chakula ilivunjwa, akageukia sanaa ya ubunifu

BONGO LA BIASHARA: Sehemu yake ya biashara ya chakula ilivunjwa, akageukia sanaa ya ubunifu

Na PATRICK KILAVUKA

INGAWA alianza usanii akiwa shule ya msingi hadi shule ya upili, Geoffrey Lubia Lugaye anasema baada ya kumaliza masomo ya sekondari, alianza kutafuta riziki kuweza kujikimu na baadaye apate malighafi ya kufanyia kazi ya usanii wa masuala ya viumbe hai na mambo ya kale kama msanii mweledi.

Ili kupata upenyo, alijiingiza katika biashara ya hoteli baada ya kupata kibanda eneo la Upperhill jijini Nairobi.

Alifanya kazi hiyo kwa miaka sita kabla vioski kubomolewa kwa sababu ya upanuzi wa barabara eneo hilo.

“Papo hapo wazo la kuimarisha talanta yangu ya usanii lilianza kunipa mshawasha wa kuchora na kutengeneza vinyago vya viumbe mbalimbali kwenye ubao maalum,” asema Lubia aliyesomea Shule ya Msingi ya Heshima, Shauri Moyo, Kaunti ya Nairobi kisha kujiunga na Shule ya Upili ya Bukhungu High, Kaunti ya Kakamega kabla kuguria Shule ya Upili ya Equator High, Thika alikohitimia.

Kwa miaka minne sasa amekuwa akifanya kazi hii akitumia vigae, mawe, magodoro au kusheni, kemikali ya maalum, rangi na kalamu ya kuchora miongoni mwa vifaa vingine.

Anatumia pia malighafi ambayo imetumiwa kuunda picha za watu, viumbe hai na vya kale kwa ubunifu mkubwa kama njia ya kuyatunza mazingira.

Msanii huyo ana uwezo wa kuchora hata michoro ya kuhamasisha kuhusu mazingira na kuyatunza.

Kwa sababu ya fikira ya kina mawazoni mwake, anasema taswira za michoro ya picha za kale hujitaswiri akilini hali ambayo humwezesha kuzichora picha zake kama vinyago kuelezea mambo au masuala ya viumbe vya kale ili vizazi vijavyo viwe na njia ya kurejelea historia na kuhamasika.

Mfano ni picha zenye ulimbwende ambazo amekwisha kuzikamilisha pichani.

Kutokana pia na masuala muhimu yanayohusu binamu na wanyama, anaweza kuyasanii.

“Kazi zangu zingine huzitengeneza kutoka kwa plastiki na ubao almradi nina hoja husika au picha,” anasema msanii Lugaye ambaye huchukua muda wa miezi saba kukamilisha kazi ya masuala ya kale na anafanyia kazi yake mkabala wa steji ya Community, Jumatatu hadi Jumamosi japo anasema usumbufu wa askari wa jijini huwa kikwazo katika utekelezaji wa kazi yake ya kujitolea.

Lubia anadokeza kwamba kwa vile kazi za usanii huwa za kumgharimu sana, bei ya kazi yake hutegemea bidii aliyotumia na malighafi.

Kwa sasa msanii huyo amezama katika masuala ya kutumia usanii kuangazia masuala ya sayansi ya hali ya anga na uharibifu wa mazingira na kurusha mtandaoni.

Anatazamia kuunda ubao mkubwa ambao unaweza kusheheni michoro ya elfu tatu hadi nne ya vinyago vya masuala mbalimbali ya kale, kisasa, ambayo yanahusu maisha ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Hata hivyo, anasema mradi kama huo huchukua muda na hela ambazo bado ni changamoto japo ndoto yake ingali hai.

Mambo mengine ambayo yangali changamoto kwake na wasanii wengine ni watalii wa humu nchini kutojitokeza kikamilifu kuwanunulia kwa wingi kazi zao za usanii hali ambayo inawafanya kukosa hela za kuwekeza katika kazi zao bunifu.

Ila, anawaomba wananchi kuwanunulia wasanii kazi zao kama njia ya kuwainua na kuwatia motisha kupanua mawazo na kujiwezesha kiriziki.

Isitoshe, anaomba wawekezaji na serikali kuwasidia wasanii kupata masoko ya kimatiafa kwani wana mengi ya kuonyesha katika ujasiriamali.

You can share this post!

Hofu IAAF ikipanga kuondoa baadhi ya mbio za Diamond

Yatani aomba seneti kuidhinisha mkopo wa hadi Sh9 trilioni

adminleo