Jumatatu sio siku ya mapumziko, Matiang'i afafanua
Na CHARLES WASONGA
WAZIRI wa Masuala ya Ndani Fred Matiang’i amefafanua kuwa Jumatatu Oktoba 28, 2019, sio siku ya mapumziko Kenya kama inavyodaiwa na baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii.
Hii ni kufuatia nakala ya notisi feki ya gazeti rasmi la serikali inayozungushwa mitandaoni kutangaza kuwa Jumatatu ni siku ya mapumziko na hivyo watu hawapaswi kwenda kazini.
Kwenye taarifa iliyowekwa katika akaunti ya Twitter ya wizara hiyo Ijumaa Dkt Matiang’i anapuuzilia mbali madai hayo na kushikilia kuwa Jumatatu ni siku ya kawaida ya kazi.
“Nawaomba mpuuzilie mbali notisi ya gazeti la serikali inazungushwa mitandaoni ikidai kuwa Jumatatu ni siku ya mapumziko. Jumatatu inasalia siku ya kazi,” wizara hiyo ikasema
Picha ya notisi hiyo feki iliibuka ikizingatia kuwa Sikukuu ya Kihindi, Diwali itaadhimishwa Jumapili Oktoba 27.
Hata hivyo, sikukuu hiyo sio miongoni mwa ile inayotambuliwa kisheria kama sikukuu nchini Kenya.
Sherehe za Diwali hudumu kwa kati ya siku nne na tano.
Sikukuu hiyo ambayo huandamanishwa na urushaji wa fataki husherehekewa na waumini wa madhehebu ya Hindu, Jians, Sikh na baadhi ya waumini wa dhehebu la Budha kila mwaka kwa heshima ya Ramachandra.