MWITHIGA WA NGUGI: Kauli kuwa ‘Vijana ndiyo viongozi wa kesho’ ni mzaha mtupu
Na MWITHIGA WA NGUGI
AMA kweli kama kuna msemo ambao umetumiwa vibaya na viongozi wetu na hususan tangu tujinyakulie uhuru wetu ni msemo kuwa vijana ndio viongozi wa kesho.
Wengi wetu tuna bahati kuwa tumeziona serikali kadha, serikali ya Hayati Mzee Jomo Kenyatta, yake mstaafu Daniel Moi na vilevile ya Rais mstaafu Emilio Mwai Kibaki na sasa serikali ya sasa inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.
Hata hivyo, Hayati Jomo angalifufuka leo angalidhani labda aliaga dunia jana kwani majina ya vigogo watajika yangali kwenye ngazi za uongozi na siasa za nchi hii.
Kila uchao wazazi wanaendelea kuwasomesha watoto wao kwenye taasisi na vyuo mbalimbali huku wakitumia pesa na mali yao kutimiza ndoto za watoto wao kwa kuufukuza ujinga, lakini la kutamausha ni kuona ni jinsi ukosefu wa ajira nchini unavyozidi kuwatokomeza vijana na wasomi wa nchi hii kwenye bahari kuu ya umasikini.
Miaka ya 2013 na 2017 itasalia katika kumbukumbu ya Wakenya wengi na hasa vijana wa taifa hili, utawala wa TNA na Jubilee mtawalia, kwenye kampeini zake rais na naibu wake waliahidi mengi mazuri ikiwemo ajira kwa mamilioni kwa vijana, jambo ambalo liliwafanya vijana kuwachagua viongozi hawa kwa matumaini kuwa maisha yao ya uchochole yangebadilika.
Ukweli mchungu ni kuwa chochote king’aacho si dhahabu; Jubilee na uongozi wake umewafanya vijana wengi kuachwa vinywa wazi na hasa kutokana na teuzi za ajira ambazo zimekuwa zikifanywa na Rais.
Ni wiki jana tu taifa lilipigwa na bumbuazi wakati rais aliwateua wazee kama si vikongwe katika nyadhifa mbalimbali za usimamizi wa mashirika ya kiserikali, jambo ambalo hadi leo linazidi kuzua midahalo mikali katika mitandao ya kijamii na mashinani.
Swali ni je, iwapo serikali itaendelea kuwapa kazi vikongwe, vijana wa taifa hili watapata kazi lini na wapi?
Ufahamu
Viongozi walioko mamlakani wanafaa kuelewa fika kwamba, kufaulu kwa taifa letu katika siku za usoni kutategemea juhudi na uwepo wa vijana wetu na ndiposa wanafaa kushirikishwa katika uongozi na katika mipango ya maendeleo ya serikali na wala si tu kuwatumia vibaya wakati wa kampeini za kisiasa.
Wakati umefika sasa kwa vijana kukataa dhana kwamba vijana ndiyo viongozi wa kesho kwani, wengi wamezeeka chini ya wito huu huku mababu zao wakiendelea kukatalia kwenye nyadhifa za uongozi na kuwanyima vijana nafasi ya kuitumikia nchi wakati wa ujana wao.
Hata hivyo, hili litawezekana tu iwapo sote tutakataa kabisa mirathi ya siasa mbaya na ukabila, jambo ambalo kwa miaka mingi limetufanya kuwachagua watoto na watoto wa wanasiasa wakongwe.