Makala

MAPISHI: Jinsi ya kuandaa burger

October 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MARGARET MAINA

[email protected]

Muda wa kauandaa: Dakika 10

Muda wa mapishi: Dakika 10

Walaji: 5

Vipande vya nyama vya kutumika katika mapishi ya Burger. Picha/ Margaret Maina

Vinavyohitajika

  • mikate 5 ya burger
  • siagi ya kukaangia mikate
  • vitunguu maji 3
  • nyanya 2
  • majani ya salad
  • parachichi
  • sauce utakazopenda (tomato sauce, mayonnaise au BBQ sauce)
  • mafuta ya kupikia
  • kilo 1 ya nyama ya kusaga
  • chumvi na pilipili manga
  • vipande 5 vya jibini

Jibini huwa ni ule mgando utokanao na maziwa ya ng’ombe yaliyotolewa maji na kugandishwa.

Mapishi ya Burger huhitaji umakinifu . Picha/ Margaret Maina

Maelekezo

Katakata kitunguu na nyanya vipande vya mduara; katakata parachichi vipande virefu.

Osha, katakata na kukausha majani ya salad kwa kutumia kitambaa cha jikoni au karatasi shashi maalumu kwa matumizi ya jikoni.

Gawanya nyama kwenye madonge matano.

Finyafinya kutengeneza umbo mduara. Nyunyizia chumvi na pilipili manga juu.

Kwenye kikaangio kilicho kwenye meko yenye moto mkali kiasi, chemsha mafuta.

Weka nyama kwenye kikaangio, upande wenye chumvi na pilipili manga kwa chini halafu pia nyunyizia chumvi na pilipili manga kwa upande wa juu.

Acha nyama iive bila kugeuzwa kwa muda wa dakika nne. Geuza ili nayo iive upande mwingine hadi jinsi utakavyopenda.

Weka jibini juu sekunde kama 30 kabla ya kutoa nyama kwenye kikaangio au mpaka iyeyuke. Funika kwa sekunde utakazoweka jibini.

Kata mkate katikati kisha upake siagi juu kwenye upande wa ndani.

Kwenye kikaangio katika meko yenye moto wa wastani, weka mkate upande wenye siagi kwa chini. Kaanga mpaka uwe wa kahawia na ukauke kiasi; angalia usiungue.

Epua mkate, pangilia nyama na viungo vingine kwenye mkate kama utakavyopenda.

Pakua na ufurahie na kinywaji chochote ukipendacho.