• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
ULIMBWENDE: Jinsi ya kuhakikisha nywele zako zinakua haraka

ULIMBWENDE: Jinsi ya kuhakikisha nywele zako zinakua haraka

Na MARGARET MAINA

[email protected]

KAMA wewe umeanza kukuza nywele na nywele zako hazikui haraka kama ulivyotegemea basi inawezekana hauzitunzi vizuri.

Nitakuelezea njia unazoweza kutumia kukuza nywele zako haraka na kukujulisha ni makosa gani ambayo yamkini umekuwa ukiyafanya yanayositisha ukuaji wa nywele zako.

Kosa la kwanza, ni kwamba watu wengi wananyoosha nywele zao mara kwa mara. Mtu akifanya hivi, ndiyo basi tena anakuwa anaziua nywele zake na zitaanza kukatika wakati wa kuchana au muda wowote. Basi inabidi upunguze kutumia vifaa kama hivi ili nywele zako zikue.

Pili, tunavyoziachia nywele na kusuka mtindo wa rasta, nywele za kawaida au kushonea ‘weave’ zinakubalika, ila ukizichana na kuzibana nywele basi hapo kuna uwezekano mkubwa kwamba zitaharibika au zitakatika.

Pia, kutokukata ncha baada ya muda, ncha zinaweza kuanza kuchanika na inabidi uzikate ili nywele zikue vizuri kwa sababu ncha huchangia kwenye kusitisha ukuaji wa nywele na kukata nywele zenyewe. Unaweza kukata ncha sentimita mbili baada ya miezi mitatu au minne.

Kutunza

Kwanza, inabidi uzisuke nywele zako mara kwa mara ili zisiharibike au zisikatike. Hivi utaweza hata kuzuia ncha zilizoharibika.

Kama hujisikii kusuka nywele au kushonea ‘weave’ basi unaweza kuzibana kwa juu au kuzifunga ukitumia kitambaa bora tu kiwe cha silk ili nywele zako zisiharibike (unaweza kukitumia hata wakati wa kulala).

Pili, inabidi upake mafuta kwenye kichwa chako mara kwa mara; hasa unapojisikia kama kichwa kimekauka au kama kinawasha. Mafuta mazuri kutumia kwa ajili ya ukuaji wa nywele ni mafuta ya nazi, castor oil, Moroccan, Jamaican au lavender. Unaweza pia kutumia mafuta mengine yoyote bora tu yasiwe ya mgando.

Pia, usizioshe nywele kwa kutumia shampoo mara kwa mara kwa sababu inaondoa mafuta kwenye kichwa na nywele zako.

Basi, inabidi uoshe nywele na conditioner kama unaona nywele zako sio chafu sana, ila kama unaona nywele zako ni chafu, basi osha ukitumia shampoo.

Itakuwa bora ukipaka mafuta kabla hujaosha nywele na uoshe nywele zako kila baada ya wiki moja na kama zinakatika, basi osha baada ya wiki mbili au tatu.

Vilevile ni muhimu kula vyakula vingi vyenye protini kama kuku, maharagwe au nyama yoyote inayokubalika.

You can share this post!

Wakanusha mashtaka 22 kuhusu ulaghai wa Sh48m za...

ULIMBWENDE: Epuka matumizi holela ya vipodozi

adminleo