• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
OBARA: Serikali ifunge madhehebu yanayoletea waumini maafa

OBARA: Serikali ifunge madhehebu yanayoletea waumini maafa

Na VALENTINE OBARA

UHURU wa kuabudu ni haki ya wananchi wa Kenya inayolindwa kikatiba.

Licha ya haya, utapeli ulioingia katika masuala ya ibada imefikia kiwango cha kutisha.

Hii ni kutokana na kuwa kando na utapeli wa kutajirisha wahubiri tuliozoea, kuna wahubiri ambao wanapotosha waumini wa madhehebu yao kwa kiasi cha kuweka maisha yao hatarini na hata kuangamia.

Wiki iliyopita kuliibuka kisa ambapo mwili wa mvulana wa miaka 13 ulipatikana nyumbani kwao. Ilisemekana mamake mtoto huyo alikuwa akimwombea kwa imani kwamba atafufuka.

Ingawa wapelelezi wangali wanafanya uchunguzi kubainisha mbivu na mbichi kuhusu kisa hicho cha kutisha, ripoti za mapema zinaonyesha mama aliyepumbazwa na kupotoshwa kidini. Sitashangaa ikipatikana mtoto huyo aliugua kwa muda mrefu na hakupelekwa hospitalini kwa sababu ya imani za mamake za kidini.

Wiki hiyo hiyo, ushahidi wa kuogofya ulitolewa kortini kuhusu mauaji ya kasisi. Ilisemekana mauaji hayo yalihusiana na utoaji wa kafara katika dhehebu la Illuminati.

Hii si mara ya kwanza ambapo tunasikia kuhusu mauaji yanayohusishwa na imani za kidini. Kuna wakati baba aliua familia yake nzima akajitoa uhai, ikaripotiwa hayo yote yalitokana na imani zake za kidini.

Wakati haya yote yanapotendeka, wananchi wengi wasio katika madhehebu hayo huweza tu kulalamika na kushangaa mbona serikali isikamate viongozi wa madhehebu hayo na kuyapiga marufuku kuendeleza shughuli zao humu nchini.

Ni kweli kwamba si rahisi kushtaki viongozi hao kwani kupata ushahidi wa kuthibitisha walipumbaza waumini wao ni vigumu mno. Hii ndio sababu wanaokamatwa wakati mwingi ni waumini waliohatarisha maisha yao au ya wenzao, sanasana maisha ya watoto wao.

Lakini serikali ina nguvu. Imetuonyesha inaweza kufanya mambo mengi bila kufuata sheria, katiba wala maagizo ya mahakama inapoamini ni kwa maslahi ya umma.

Serikali imewahi kutuonyesha inaweza kuamua kufunga makanisa ikidai inahofia kutatokea vurugu, hata kama jambo la busara lingekuwa kutoa ulinzi kwa waumini dhidi ya watu wachache ambao wangetokea kuvuruga ibada.

Kwa msingi huu, naamini serikali ikitaka, inaweza kufunga mara moja madhehebu hayo ambayo ni wazi yanazidi kusababisha maafa ya wananchi wasio na hatia.

Madhehebu yanayopinga watoto kupata chanjo, waumini kupokea matibabu hospitalini, yanayodai kuwa na uwezo wa kutenda miujiza ilhali inaonekana wazi ni utapeli, na yale yanayoshawishi wagonjwa mahututi kutolewa hospitalini ili wakaponywe lakini hufariki katika viwanja vilivyojaa baridi, ni hatari kwa usalama wa raia.

Uhuru wa kuabudu, sawa na aina yoyote nyingine ya uhuru uliolindwa kikatiba haufai kuvuka mpaka. Isiwe ni uhuru unaofikia kiwango cha kusababisha maafa kwani haki ya maisha ni kuu zaidi sio kikatiba pekee bali pia mbele za Maulana.

You can share this post!

KAMAU: Trump anairejesha dunia enzi za giza

Nairobi City Stars yazidi kutesa ligi ya NSL, Ushuru FC...

adminleo