Makala

MAPISHI: Jinsi ya kuandaa nyama ya mishikaki

October 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MARGARET MAINA

[email protected]

Muda wa kuandaa: Dakika 15

Muda wa ku-marinate: Dakika 30 au usiku kucha

Muda wa kuchoma: Dakika 10

Walaji: 8

Vinavyohitajika

  • kilo 1 ya nyama ya ngómbe isiyo na mifupa
  • ¼ kikombe sukari ya kahawia
  • ¼ kikombe soya sosi
  • kijiko 1 cha kitunguu saumu
  • kijiko 1 cha tangawizi
  • pilipili
  • chumvi ¼ kijiko
  • cornflour ½ kijiko

Kwa mishikaki

  • pilipili mboga za rangirangi (kijani, njano, nyekundu)
  • kitunguu maji 1
  • vipande vya mananasi
Mishikaki. Picha/ Margaret Maina

Maelekezo

Osha, katakata na kukausha nyama halafu menya na twanga kitunguu saumu na tangawizi.

Kwenye sufuria ndogo, changanya sukari, soya sosi, juisi ya nanasi, kitunguu saumu, tangawizi, pilipili na chumvi. Chemsha huku ukikoroga moto wa wastani mpaka sukari iyeyuke.

Kwenye bakuli ndogo, koroga mchanganyiko wa vijiko viwili vya maji na cornflour.

Ongeza mchanganyiko huo kwenye sufuria. Acha mchanganyiko uchemke mpaka uanze kuwa mzito. Epua, weka kando ipoe.

Acha sosi ipoe, weka kiasi cha robo kikombe pembeni utakayoitumia baadaye. Changanya nyama na sosi iliyobakia vizuri kwenye bakuli. Funika kisha weka kwenye jokofu viungo vikolee kwa muda wa nusu saa au usiku kucha.

Ukiwa tayari kupika, katakata pilipili mboga, kitunguu na nanasi vipande vya mraba. Ongeza mafuta ya kupikia na changanya vizuri.

Dunga nyama na mchanganyiko wa nanasi na pilipili mboga kwenye vijiti vya mishikaki huku ukichanganyachanganya.

Choma kwa muda wa dakika 10 au mpaka nyama iive. Kwa ovena, oka mishikaki kwa dakika 30. Paka sosi iliyobakia kwa juu wakati unageuza mishikaki ishike vizuri.

Pakua na ufurahie.