Waziri Matiang’i afungua KCPE kwa maombi
Na WAANDISHI WETU
WAZAZI wa shule kadhaa Jumanne walijitokeza kwa hasira ilipofichuka wasimamizi wa shule ambazo watoto wao wamekuwa wakijiandaa kwa Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE) waliwasajili kwingineko.
Katika Kaunti ya Kakamega, wazazi wa watahiniwa 70 katika Shule ya Msingi ya Mumias walisema walisema hiyo ni njama ya wasimamizi wa shule kuzuia alama ya jumla ya matokeo ya KCPE kushuka ili kujitafutia sifa.
“Shule ina watahiniwa takriban 200 na ni 130 pekee waliosajiliwa kufanya mtihani huko,” akasema Tawakal Burhan ambaye ni mzazi.
Watahiniwa 50 walipelekwa katika kituo cha watahiniwa wa kibinafsi huku wengine 20 wakisajiliwa katika Shule ya Faith Academy.
Afisa wa elimu katika Kaunti Ndogo ya Mumias, Bw Francis Shikanda alithibitisha kupokea malalamishi hayo na kuanzisha uchunguzi.
Katika Kaunti ya Kisumu, wazazi walivamia Shule ya St Anne Academy wakidai shule ilisajili watahiniwa 20 pekee kati ya wanafunzi 46 wa Darasa la Nane. Ilisemekana waliosalia walisajiliwa kisiri katika shule ya umma.
Mkurugenzi wa Elimu katika Kaunti ya Kisumu, Bw Isaak Atebe alisema walipokea malalamishi hayo na kutuma maafisa kuchunguza shule hiyo.
Mtihani wachelewa kuanza
Katika Shule Msingi ya NYS Gilgil, Kaunti ya Nakuru mtihani ulichelewa kuanza kwa takriban dakika 30 baada ya Waziri wa Usalama wa Nchi, Dkt Fred Matiang’i kuagiza watahiniwa wahamishwe.
Kabla waanze mtihani wao, Dkt Matiang’i aliwaombea pamoja na watahiniwa wengine wote kitaifa.
Kuta za jengo hilo zilikuwa na nyufa na madirisha yaliyovunjika vioo zamani yakizibwa na karatasi. Ilibidi wahamishwe hadi madarasa mengine shuleni humo.
Wasichana kadhaa walijifungua huku watahiniwa wengine wengi wakifanya mitihani yao hospitalini walikolazwa kwa magonjwa mbalimbali.
Visa vya wasichana kujifungua viliripotiwa katika Kaunti za Taita Taveta, Pokot Magharibi na Kitale.
Waziri wa Elimu, Prof George Magoha alidokeza kuna wasichana wengine ambao ni wajawazito, akisema wizara hiyo imepanga ambulensi zitakazotumika kusaidia baadhi yao endapo watajifungua.
Ingawa mikakati iliyowekwa na serikali kukabiliana na changamoto za mafuriko ilionekana kufua dafu katika maeneo mengi, bado mitihani ilicheleweshwa na hali mbaya ya barabara katika maeneo kadhaa.
Miongoni mwao ni shule za Kaunti Ndogo ya Moyale, Kaunti ya Marsabit ambapo kulikuwa na helikopta moja iliyotegemewa kusafirisha karatasi za mtihani huo baada ya barabara kuharibiwa na mafuriko.
Mkurugenzi wa Elimu katika kaunti hiyo, Bw Paul Mwongera alisema shule zilizoathirika ni Dabel, Kinisa, Yaballo, Godoma, Nana na Bori.
Katika Kaunti ya Tana River, vituo vitano vya mitihani vilipelekewa karatasi zao kwa boti baada ya daraja linalounganisha shule na kituo cha kuhifadhi mitihani kusombwa na maji ya Mto Tana.
Wasimamizi sita wa mtihani walipata ajali Marsabit gari lao lilipobingiria. Watatu kati yao walilazwa katika Hospitali ya South Horr.
Katika Kaunti ya Homa Bay, gurudumu la basi lililokuwa likisafirisha mitihani liling’oka na kulazimu maafisa kutafuta basi lingine.
Ripoti za: Valentine Obara, Samuel Baya, Lucy Mkanyika, Mishi Gongo, Jacob Walter, Stephen Oduor, Gerald Bwisa, George Odiwuor na Shaban Makokha