Jaji azuia bajeti ya mahakama kupunguzwa
Na MAUREEN KAKAH
IDARA ya Mahakama imepata afueni baada ya Mahakama Kuu kusimamisha hatua ya serikali ya kupunguza bajeti yake.
Jaji Makau Mutua jana alitoa agizo hilo katika kesi ambayo Chama cha Mawakili Kenya (LSK), kimeshtaki Wizara ya Fedha na Mwanasheria Mkuu kufuatia hatua ya kupunguza bajeti ya Mahakama.
Jaji Makau alisimamisha kwa muda Wizara ya Fedha kupunguza kwa vyovyote bajeti ya Mahakama na akaitaka Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC) kutoa ripoti ya kina kuonyesha jinsi kupunguzwa kwa bajeti kumeathiri utoaji wa haki.
“Kabla ya kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi hii, agizo limetolewa kuzuia wizara ya fedha, maajenti wake, maafisa au watu wengine kutekeleza ilani iliyotolewa Septemba 24 au kutoa maagizo yasiyofaa kuhusiana na bajeti ya mahakama,” Jaji Makau alisema.
Septemba 2019, Kaimu Waziri wa Fedha, Ukur Yatani, alitoa agizo la kupunguzwa kwa bajeti ya Mahakama kwa asilimia 50.
Mnamo Oktoba 9, 2019, Msajili Mkuu wa Mahakama Anne Amadi aliandika ilani kwa wakurugenzi, wasajili na wakuu wa idara zote katika mahakama kuwataka watekeleze agizo hilo.
Kulingana na barua hiyo, mahakama zote za kuhama hama na majopokazi ya mahakama zilisitishwa huku wiki ya huduma ambayo majaji na mahakimu walitumia kuharakisha kesi zikifutiliwa mbali.
Katika kesi yake, LSK inasema kupunguzwa kwa bajeti ni kuingilia uhuru wa mahakama na kuvuruga utoaji wa haki kwa Wakenya.
Mahakama haikuweza kufadhili miradi yake ipasavyo baada ya kutengewa nusu ya pesa ilizoomba kwenye bajeti ya mwaka 2019.
Idara hiyo ilikuwa imekadiria kutumia Sh19.8 bilioni kwa mishahara, Sh11.4 bilioni kwa miradi ya maendeleo na Sh891 milioni za JSC.
LSK imetaja seneti, JSC, Bunge la Taifa na Shirika la International Commission of Jurists Kenya, kama wahusika katika kesi hiyo.
Jaji Makau aliagiza kesi hiyo kutajwa Novemba 6.