Makala

UCHAMBUZI WA VITABU VYA FASIHI: Maudhui zaidi katika tamthilia ya Kigogo

October 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na WANDERI KAMAU

Matumizi mabaya ya vyombo vya serikali

KUTOKANA na ushawishi wake mkubwa, Majoka anatumia vibaya vyombo vya utawala wake kuwahangaisha watu ambao wanakataa kutii kanuni na masharti anayowawekea.

Kwa mfano, anatumia polisi kuwatawanya waandamanaji na kuwaumiza wapinzani wake. Kwenye kizaazaa kinachotokea katika Soko la Chapakazi, Tunu anaumizwa mguu.

Runinga ya Mzalendo inahangaishwa na utawala wa Majoka kwa kuangazia maandamano yanayotokana na utawala wake dhalimu.

Hataki maovu hayo yaangaziwe, kwani anahofia kwamba hilo litamharibia sifa. Anafunga vituo vyote vya habari vinavyoikosoa serikali yake.

Ni kituo kimoja pekee kinachobaki, ambacho anakitumia kueneza uwongo kuhusu hatua na mafanikio yaliyofikiwa na utawala wake.

Hatua ya kufungwa kwa Runinga ya Mzalendo inatokana na ushauri ambao Majoka anapata kutoka kwa Kenga, ambaye ni mmoja wa washauri wake wakuu anaowaamini sana.

Majoka anakilazimisha kituo kinachobaki kupeperusha nyimbo za kumsifu yeye binafsi na utawala wake.

Miongoni mwa habari za potoshi zinazopeperushwa ni kwamba Tunu hawezi kupigania haki za Wasagamoyo kwani amelemazwa mguu.

Mauaji

Mojawapo ya mbinu anayotumia Majoka kuwakabili wakosoaji wake ni kupanga mauaji ya kikatili dhidi yao.

Hii ni mbinu ambayo imekuwa ikitumiwa na viongozi wengi wa kiilma katika nchi nyingi barani Afrika.

Vijana watano wanauawa watu wanapoandamana katika kampuni ya Majoka. Mtindo wa mauaji unaonekana kuwa hali ya kawaida katika jimbo la Sagamoyo.

“Natumai kwamba hakuna aliyeuliwa, sitaki kujipaka matope tena” (uk31). Ni kauli anayotoa Majoka akionekana kujuta kutokana na mauaji yanayoendelea.

Kifo cha Jabali kilipangwa katika ajali kwa kuwa mpinzani wa Majoka. Chama chake cha Mwenge kinasambaratishwa mara tu baada ya kifo chake.

Tunu anamwambia Majoka kuwa yeye na wenzake ni wauaji (uk43). Majoka anapuuza kauli hiyo kwa kejeli.

Inavyoibuka katika tamthilia hii, mauaji yanaonekana kuwa vitendo vya kawaida kwa utawala wa Majoka. Tunu anamwambia Majoka kuwa atalipa kila tone la damu alilomwaga Sagamoyo. Hili linaashiria kuwa kuna watu wengi wanaouawa na utawala huu. Babake Tunu anakufa katika Majoka and Majoka Company baada ya kutendewa ukatili na Marara na watu wake.

Hashima anasema kuwa damu nyingi imemwagika Sagamoyo hadi ardhi imeingia najisi. Mashujaa walifariki wakati wakipigania uhuru wa Sagamoyo. Mhusika Ngurumo naye ananyongwa na chatu akitoka Mangweni.

Majoka anapanga kutekeleza mauaji kwa kumwondoa chatu mmoja ili pawe na usalama katika jimbo hilo. Kifo cha Ngao Junior kinatokea ambapo anapatikana katika uwanja wa ndege akiwa na sumu ya nyoka.

Majoka anasema kuwa ziwa kubwa limefurika damu furifuri, kumaanisha kuwa vifo vya watu wengi vimetokea Sagamoyo. Kutokana na ukatili wake, watu wanalilia damu ya Majoka wakitaka kumuua (uk79).

Ufisadi

Serikali ya Majoka ni fisadi. Mfano mmoja wa ufisadi huu ni pale serikali ya Majoka inampa Mamapima kibali cha kuuza pombe haramu licha ya kufahamu athari zake kwa watu anaowauzia. Mamapima pia ni fisadi kwani anawapunja walevi bila wao kufahamu, hasa wanapolewa.

Majoka anatumia pesa za umma visivyo kugharimia njama ili kuzima uchunguzi anaoendesha Tunu kuhusu ajali anayopata Jabali.

Kijumla, viongozi katika jimbo hili wanaibukia kuwa wafisadi. Mfano unadhihirika katika visa vingi wanapowaitisha wananchi hongo (kitu kidogo). Wakati mwingine wanadai kitu kikubwa au kitu chote (uk3). Bila shaka, hili linaashiria jinsi ufisadi ulivyoenea katika jimbo hilo.

Viongozi wanatumia mali ya umma visivyo kufadhili miradi ambayo si muhimu. Mfano ni pale Majoka anatenga fedha ili kufadhili mradi wa kuchonga vinyago ilhali hauna manufaa yoyote kwa wananchi. Kinaya ni kwamba mradi huo unajengwa wakati ambapo kuna malalamishi makubwa kuhusu udhalimu unaoendeshwa na serikali hiyo, kama kuwafurusha wananchi kutoka Soko la Chapakazi. Kinaya kingine ni kuwa unajengwa kama mojawapo ya mikakati ya kusherehekea uhuru wa jimbo hilo.

Majoka anafisidi wananchi wa Sagamoyo ili ajenge hoteli ya kifahari. Anafanya hivyo bila kujali hali mbaya ya soko. Soko la Chapakazi ni chafu ilhali wananchi wanalipa kodi ya kulisafisha. Majoka anadai kuwa ana mradi muhimu (hoteli) kuliko kulisafisha soko. Majoka pia alikuwa na mpango wa kumpa Ashua kazi ya ualimu katika Majoka and Majoka Academy kwa njia isiyo halali. Hii ni mifano tu inayodhihirisha jinsi ufisadi umetaasisika katika utawala wa Majoka.

Usaliti

Majoka anawasaliti Wanasagamoyo. Watu wote wanamlaumu kwa kuwasaliti licha ya kuwa kiongozi wao. Anatumia polisi kuwahangaisha Wanasagamoyo badala ya kulinda usalama wao kwani ndiye kiongozi.Kingi anamsaliti Majoka wakati wa mwisho, wakati anapinga amri yake kwamba watu wapigwe risasi. Hii ni ikizingatiwa kuwa siku zote alikuwa akitii kauli na amri zote za Majoka.Majoka vile vile anawasaliti Wanasagamoyo kwa kupanga mauaji yao badala ya kulinda na kutetea haki zao kama kiongozi wao. Huu ni usaliti wa kufadhaisha, ikizingatiwa kuwa kiongozi anapaswa kutumia uwezo kuwalinda wananchi wake badala ya kupinga njama za kuwaua.

Ashua anamsaliti Sudi kwa kuomba talaka licha ya Sudi kumpenda kwa dhati. Usaliti pia unajitokeza miongoni mwa wanandoa kadhaa waliorejelewa tamthiliani.

Usaliti mwingine unadhihirika pale wahusika Boza na Kombe wanawasaliti wanamapinduzi kwa kuunga mkono Majoka na uongozi wake. Wanafanya hivi licha ya kufahamu mateso ambayo wananchi wanapitia chini ya uongozi wa Majoka.

Majoka anamsaliti Husda kwa kukiri kuwa hampendi licha ya kuwa mkewe. Ndoa kati ya Majoka na Husda ni miongoni mwa zile ambazo zinakumbwa na matatizo tamthiliani.

Utabaka

Jimbo la Sagamoyo limegawika katika matabaka mawili; tabaka la watawala na tabaka la watawaliwa. Mfano wa watawala ni watu kama Majoka. Wanaishi maisha ya kifahari bila kujali hali za watu wanaowatawala; ambao wanaishi maisha ya kimaskini na mahangaiko kila siku.

Maslahi ya watawala yanashughulikiwa kwa dharura. Kwa mfano, wakati Majoka anapozirai, daktari wake anaitwa kwa haraka.