KINA CHA FIKIRA: Watahiniwa walenge kuvuna walichopanda, maisha hayaishii hapo
Na KEN WALIBORA
WANAFUNZI wa darasa la nane nchini Kenya wamejibwaga kwenye ulingo ili kufanya mtihani wa taifa wa KCPE nchini Kenya.
Kwa wengi wao hii ndiyo mara ya kwanza kabisa kuwahi kufanya mtihani mkubwa kama huo. Kwa hiyo nyoyo zinawadunda na majasho kuwatoka kwapani na vipajini. Mtihani ni mtihani hata ukiwa mtihani wa maisha.
Kwa hiyo kiwewe wanachokuwa nacho kinaeleweka kabisa. Wameambiwa tangu hapo kwamba mustakabali wao unategemea matokeo ya mtihani huo. Mtihani huo unaamua hatima ya maisha yao yote. Kweli?
Mimi sina tajiriba ya kuufanya mtihani wa darasa la nane KCPE. Nilisoma mfumo mwingine tofauti, mfumo wa 7-4-2-3 ambao uliutangulia ule wa 8-4-4.
Kutokana na hilo ni rahisi mtu kuhitimisha kwamba siwezi kutoa kauli mwafaka kuhusu watahiniwa. Lakini hata mtihani wangu wa kwanza wa CPE niliofanya ujanani, ulikuwa pia mtihani, sawa na mitihani mingine ya maisha ambayo nimekumbana nayo katika aushi yangu.
Ninachoelewa ni kwamba kwa mwanafunzi, huu ni wakati wenye utata na utatanishi. Lakini ajabu ni kuwa mara nyingine walio na wasiwasi zaidi ni wazazi na walimu.
Baadhi yao wana desturi ya waume wanaopata uchungu wa kuzaa kuliko wake zao waja wazito. Unamwona mwanamume amepatatika mkewe akiingia chumba cha kujifungulia, utadhani yeye mwanaume ndiye anayejifungua.
Mimi ndilo naliona kuwa baya kwetu. Wizi mwingi wa mitihani ya taifa unatokana na wasiwasi wa wazazi na walimu uliopindukia ule wa wanafunzi. Mwalimu mmoja mkuu aliniambia jinsi ambavyo wenzake wengine huwaita wazazi na kuwaambia, “unataka mwanao asomee shule ya Alliance au Busakala?” Hapana shaka wazazi wengi wanataka watoto wao wajiunge na Alliance wanapohitimu masomo ya shule ya msingi. Kisha, yule mwalimu mkuu akanieleza, “wenzako hao humwambia mzazi atoe kitu kidogo ili apate fununu ya yatarajiwayo kwenye mtihani.
Huu moja kwa moja unaonekana kuwa uozo, au dalili ya uozo katika jamii yetu. Kidonda kinapooza kinamnukia mwenyewe? Waswahili walisema “chako ni chako kikioza kikaushe.” Wapo wanaofunika uozo huu wa kidonda katika kile wanachokiita ubashiri wa kijacho kwenye mtihani. Hata mwaka huu, utawaona waheshimiwa wengine wakiandika kile wanachokiona kama mada ya insha itakayoletwa kwenye mtihani. Wanaweza hata kuandaa warsha na makongamano kuhusu insha tarajiwa. Pema hapo?
Mwanafunzi aliyejiandaa vilivyo anaweza kuhangaika kujua nini mada ya insha italetwa kwenye mtihani? Nikidhani kwa kipindi cha masomo yake ya shule ya msingi mwalimu amemfundisha stadi za kuandika insha na kwa hiyo anaweza kuandika insha kuhusu chochote na lolote ifaavyo. Je, inawezakana kwamba baadhi ya insha zinazoandikwa zimekaririwa neno kwa neno na kwamba wanafunzi hao wamegeuzwa mashine ya kutolesha nakala tu? Je, tunaandaa wanafunzi au fotokopia?
Nawatakia wanafunzi wote wa shule za msingi mafanikio kwenye mtihani wao. Nawapa mkono wa tahania wale wote wanaozikataa juhudi za kibwete za kuwabashiria mada ya insha.