• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
MATHEKA: ‘BBI’ ya mwananchi ni ile ambayo itaimarisha ugatuzi

MATHEKA: ‘BBI’ ya mwananchi ni ile ambayo itaimarisha ugatuzi

Na BENSON MATHEKA

MAONI yametolewa kuhusu ripoti ya jopokazi la BBI hata kabla ya kutolewa rasmi.

Kuna wanaohisi kwamba BBI inalenga kubuni nafasi za kazi kwa watu wachache na kuna wale ambao wametoa masharti kabla ya kuikubali.

Hata hivyo, kile kimejitokeza ni kuwa wote hao wanatetea maslahi yao.

Wengi wale ambao wamekimbilia kutoa maoni yao ni wanasiasa ambao kama fisi hufikiria kwanza maslahi yao kabla ya yale ya mwananchi.

Lakini cha muhimu ni kuwa ripoti hiyo inapaswa kukubaliwa na kila mtu ikiwa itakuwa na mapendekezo ya kuimarisha ugatuzi.

Viongozi wakuu wa serikali na wanasiasa wamekuwa wakisema kwamba wamejitolea kulinda ugatuzi na huu ndio wakati mwafaka wa kudhihirisha haya kwa vitendo.

Viongozi wakuu wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta wanapaswa kutumia BBI kuondoa shaka kuwa ugatuzi unahujumiwa .

Kwa mfano sekta ya afya imevurugika katika kaunti nyingi kwa sababu hakuna nia njema katika serikali kuu.

Huu ndio wakati wa kuhakikisha kwamba serikali inatengea serikali za kaunti pesa za kutosha kuimarisha sekta hii na kuimarisha maendeleo mashinani ili kila Mkenya popote alipo ahisi kuwa amenufaika.

Pia pendekezo la kufanya Seneti kuwa na nguvu zaidi linapaswa kushirikishwa katika BBI ikiwa viongozi hao wakuu wanataka kukuza ugatuzi ili kuepuka mizozo kuhusu ugavi wa mapato kama ulioshuhudiwa kwenye bajeti ya mwaka huu.

Jukumu la Seneti ni kulinda ugatuzi kwa kuchunguza utendakazi wa magavana na madai ya Wabunge kila mara kwamba maseneta hawajui kazi yao ni kupotosha Wakenya.

BBI inapasa kurekebisha hali hii ili kulinda ugatuzi na ikiwa kweli viongozi wa kisiasa wamejitolea kulinda ugatuzi, wanapaswa kuipa nguvu Seneti ili kuepuka mizozo.

Viongozi wasiweke visiki katika BBI iwapo itatoa nafasi ya kupeleka pesa zaidi mashinani.

Kwa vile mojawapo wa masuala ambayo kamati hiyo ilipaswa kushughulikia ni kuangamiza ufisadi na yeyote anayepiga juhudi za kupiga vita uovu huu ni adui wa Kenya. Kupitia BBI hatua kali zinapaswa kuchukuliwa wahusika.

Hali ya baadaye ya kustawisha nchi hii iko katika ugatuzi na kila Mkenya mzalendo anafaa kusimama kuutetea na kuulinda.

Ikiwa BBI itazingatia masuala haya itakuwa ni mwokozi ambaye nchi hii imesubiri kwa miaka mingi.

You can share this post!

TAHARIRI: Mabadiliko makubwa yafanywe katika KFS

Sarah Cohen ataka achukue nguo katika makazi yanayotajwa...

adminleo